Kibaha. Uongozi wa Manispaa ya Mji wa Kibaha Mkoa wa Pwani umewapongeza walimu wa shule za msingi na sekondari kufuatia kupanda kwa kiwango cha ufaulu katika mitihani ya kitaifa ya mwaka 2025, hatua iliyoambatana na utoaji wa tuzo kwa walimu waliofanya vizuri.
Takwimu za elimu zinaonesha ongezeko la ufaulu katika ngazi zote kuanzia upimaji wa darasa la nne, mtihani wa kumaliza elimu ya msingi hadi kidato cha nne, hali iliyochochea mamlaka za wilaya kutoa pongezi kwa walimu hao.
Kwa mujibu wa takwimu hizo, matokeo ya upimaji wa darasa la nne mwaka 2025 yameongezeka kwa asilimia 1.65 kutoka asilimia 96.20 mwaka 2024 hadi asilimia 97.85 mwaka 2025.
Katika elimu ya msingi, ufaulu umeendelea kuimarika kwa miaka miwili mfululizo ambapo mwaka 2024 na 2025 Manispaa imepata asilimia 99.52, ikiwa ni juu ya lengo la kitaifa la asilimia 85.
Kwa upande wa sekondari, matokeo ya mtihani wa kidato cha pili mwaka 2025 yameongezeka kwa asilimia 3.17 kutoka asilimia 93.94 mwaka 2024 hadi asilimia 97.11 mwaka 2025.
Aidha, matokeo ya kidato cha nne nayo yamepanda kwa asilimia 2.44 kutoka asilimia 96.30 mwaka 2024 hadi asilimia 98.74 mwaka 2025, yakionesha mwenendo chanya wa ufaulu katika ngazi zote za elimu.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi tuzo kwa walimu iliyofanyika leo Aprili 16, 2026 mjini Kibaha, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson Saimon amesema mafanikio hayo yanatokana na juhudi kubwa za walimu pamoja na usimamizi mzuri wa sekta ya elimu.
“Dhamira ya wilaya ni kuendelea kuimarisha na kupandisha viwango vya elimu kila mwaka. Walimu mna jukumu la kuendeleza juhudi hizi ili kuhakikisha wanafunzi wanapata matokeo bora zaidi,” amesema Saimon.
Ameelekeza wakurugenzi na wakuu wa shule kuendelea kutoa motisha kwa walimu katika ngazi zote ili kuongeza ari ya kufundisha na kujifunza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa ya Mji wa Kibaha, Dk Rogers Shemwelekwa amesema utoaji wa motisha umetokana na kutambua mchango mkubwa wa walimu katika kuinua viwango vya elimu.
Amesisitiza kuwa pamoja na kufundisha masomo ya darasani, walimu wanapaswa kuzingatia pia malezi ya maadili kwa wanafunzi.
“Walimu msijikite tu kwenye masomo ya darasani, bali fundisheni pia maadili mema ili kujenga jamii imara yenye nidhamu na uwajibikaji,” amesisitiza Dk. Shemwelekwa.
Naye kiongozi kutoka Taasisi ya Elimu WIPAHS iliyoko Kibaha Mpakani, Shabbir Hussein Khalfan amesisitiza umuhimu wa maadili kwa wanafunzi akieleza kuwa msingi wa mafanikio ya elimu si ufaulu wa kitaaluma pekee bali pia malezi bora ya tabia.
“Ni muhimu kwa walimu kuhakikisha wanafunzi wanalelewa katika misingi ya maadili mema, kwani elimu bila maadili inaweza kuligharimu taifa,” amesema Khalfan.
Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa elimu pamoja na walimu kutoka shule za msingi na sekondari za Manispaa ya Kibaha.