Dodoma. Mbunge wa Chemba (CCM), Kunti Majala, akiitaka Serikali kuchukua tahadhari juu ya mikopo inayotolewa kwa vijana wanaonunua pikipiki, akionya kuwa siku zijazo Taifa linaweza kubeba mzigo wa kuwahudumia wakopaji watakaopata ulemavu.
Majala ametoa kauli hiyo leo, Ijumaa Aprili 17, 2026, alipouliza swali la nyongeza bungeni.
Ameeleza kuwa kutokana na changamoto ya ajira, vijana wengi wamejiingiza katika biashara ya usafirishaji kwa kutumia bodaboda.
Hata hivyo, amesema wengi wao huanza wakiwa na afya njema lakini baadaye hupata ulemavu kutokana na ajali na mazingira ya kazi hiyo.
Kutokana na hali hiyo, ameitaka Serikali kueleza imejipangaje kukabiliana na changamoto ya kuwahudumia watu watakaopata ulemavu siku zijazo kutokana na shughuli hizo.
Akijibu hoja hiyo, Serikali imesema tahadhari iliyotolewa na mbunge huyo ni ya msingi na inapaswa kuzingatiwa katika utoaji wa mikopo.
Imeongeza kuwa kuna umuhimu wa kuangalia namna bora ya kubuni na kuwezesha fursa za ajira kwa vijana ambazo hazina viashiria vya madhara ya baadaye.
Katika swali la msingi, Mbunge wa Bukoba Vijijini (CCM), Dk Jasson Rweikiza, amehoji ni lini Serikali itakuja na mpango madhubuti wa kuhakikisha vijana wanapata ajira za kutosha.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Rahma Kisuo amesema Serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kukuza ajira kwa vijana.
Ameeleza kuwa mikakati hiyo inahusisha ubunifu na utekelezaji wa programu maalumu zinazowawezesha vijana kupata ujuzi na kushiriki kikamilifu katika sekta zinazozalisha ajira kwa wingi.
“Aidha, Serikali inaendelea kukamilisha mapitio ya Sera ya Taifa ya Ajira ya mwaka 2008 kwa lengo la kupanua fursa za ajira. Vilevile, inawekeza katika ujenzi wa miundombinu ya miradi ya kimkakati inayochochea ukuaji wa uchumi na hivyo kuongeza nafasi za ajira,” amesema Kisuo.
Ameongeza kuwa Serikali imeanzisha Programu ya Taifa ya kukuza ujuzi inayolenga kuwezesha nguvu kazi kupata ujuzi unaohitajika katika soko la ajira. Hadi sasa, amesema jumla ya Watanzania 168,657 wamenufaika na programu hiyo.
Pia, Serikali inaendelea kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa vijana kupitia mapato ya ndani ya halmashauri pamoja na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.
Vilevile, amesema Serikali inaratibu upatikanaji wa fursa za ajira nje ya nchi kwa njia rasmi, salama na zenye manufaa, ambapo vijana 6,367 wamenufaika katika mwaka 2025/26.
Sambamba na hayo, Serikali inatoa mikopo yenye masharti nafuu kwa vijana kupitia mapato ya ndani ya halmashauri na mfuko wa maendeleo ya vijana, pamoja na kuboresha Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura ya 410, inayotoa upendeleo wa asilimia 30 katika ununuzi wa Serikali kwa makundi maalumu yakiwemo vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
