Dar es Salaam. Kwenye familia yoyote ile, nafasi ya mwanamke huanza kujengwa tangu akiwa utotoni. Mtoto wa kike anapopewa malezi sahihi, hujengwa kuwa mama bora, mlezi makini na nguzo ya maadili katika familia.
Hivyo basi, suala la kumlea binti si jambo la kawaida bali ni uwekezaji wa moja kwa moja katika mustakabali wa familia na watu wanaoizunguka.
Wataalamu wa masuala ya malezi wanasisitiza kwamba, msingi wa kwanza katika malezi ya mtoto wa kike ni kumjengea maadili imara. Hapa ndipo anapojifunza kuhusu heshima, nidhamu na uwajibikaji.
Binti anayekuzwa katika misingi ya kujiheshimu na kuwaheshimu wengine, hukua akiwa na uwezo wa kufanya uamuzi sahihi hata anapokuwa mbali na wazazi wake. Maadili haya yanapaswa kufundishwa kwa vitendo zaidi kuliko maneno, kwa kuwa watoto huiga yale wanayoona katika mazingira yao ya kila siku.
Sambamba na hilo, wazazi wanapaswa kukumbuka kwamba elimu ina nafasi kubwa katika kumjenga mtoto wao wa kike. Elimu inayozungumziwa hapa si ya darasani pekee, bali pia elimu ya maisha. Binti anapaswa kufundishwa namna ya kujitegemea, kupanga maisha yake na kukabiliana na changamoto mbalimbali.
Hii inamjenga kuwa mwanamke mwenye kujiamini, anayeweza kusimamia familia na kushiriki katika maendeleo ya jamii. Mama bora wa kesho ni yule anayechanganya maarifa ya darasani na hekima ya maisha ya kila siku.
Aidha, malezi ya kihisia ni jambo lisilopaswa kupuuzwa. Mtoto wa kike anahitaji kukuzwa katika mazingira yenye upendo, usikivu na mawasiliano ya wazi. Wazazi wanapaswa kumpa nafasi ya kueleza hisia zake na kujifunza namna ya kuzidhibiti.
Hali hii humsaidia kukua akiwa na utulivu wa akili na uwezo wa kujenga uhusiano wenye afya. Mama anayeelewa hisia zake huwa na uwezo mkubwa wa kulea watoto wake kwa upendo na busara.
Jambo lingine muhimu ni kumjengea binti uwezo wa kujitegemea. Wazazi pia wanapaswa kumfundisha kuwajibika tangu akiwa mdogo kwa kumpa majukumu yanayolingana na umri wake.
Hii humsaidia kuelewa thamani ya kazi na umuhimu wa kuchangia katika familia. Binti anayelelewa kwa mtindo wa kutegemea kila kitu kutoka kwa wazazi, anaweza kukosa uthabiti wa maisha ya baadaye.
Kinyume chake, anayefundishwa kujitegemea hukua akiwa na ujasiri wa kukabiliana na changamoto za maisha.
Katika malezi haya, ni muhimu pia kuepuka mitazamo inayomdhoofisha mtoto wa kike. Watu wengi wamekuwa na dhana zinazomwekea mipaka binti, zikimzuia kufikia uwezo wake kamili.
Lakini inapaswa kukumbuka kwamba malezi bora yanapaswa kumpa uhuru wa kuchunguza vipaji vyake na kufuata ndoto zake, huku akiongozwa na maadili sahihi. Hii humsaidia kukua akiwa na mtazamo chanya kuhusu maisha na nafasi yake mbele ya macho ya watu.
Malezi ya kiimani na kiroho nayo yana mchango mkubwa katika kumjenga mtoto wa kike. Kumfundisha juu ya uadilifu, uwajibikaji na hofu ya Mungu au dhamira njema humsaidia kuwa na dira ya maisha.
Hii ni nguzo muhimu katika kumjenga mama ambaye ataongoza familia yake kwa misingi ya haki na uadilifu.
Vilevile, wazazi wanapaswa kutambua kuwa wao ni walimu wakuu wa watoto wao. Mtoto wa kike hujifunza zaidi kupitia matendo ya wazazi wake kuliko maelekezo wanayompa.
Mama anayemwonyesha binti yake namna ya kujiheshimu, kufanya kazi kwa bidii na kuishi kwa uadilifu anampa somo la maisha lisilosahaulika.
Kwa upande mwingine, baba naye ana nafasi ya kipekee ya kumjengea binti kujiamini na kujitambua, hasa katika kuelewa thamani yake na namna ya kujiheshimu katika uhusiano.
Hata hivyo, malezi yanayozingatia ukali kupita kiasi au hofu hayana matokeo chanya. Kumbuka, binti anayelelewa katika mazingira ya vitisho au ukandamizaji, anaweza kukosa kujiamini na kushindwa kufanya uamuzi sahihi. Hivyo ni muhimu kwa wazazi kuweka mizani kati ya nidhamu na mawasiliano ya wazi, ili mtoto ajisikie salama kueleza mawazo na changamoto zake.
Hii inatukumbusha kwamba, kumlea mtoto wa kike ili aje kuwa mama bora wa kesho, ni jukumu linalohitaji uangalizi, uvumilivu na maarifa.
Na ni mchakato unaojumuisha kumjenga kimaadili, kielimu, kihisia na kijamii. Jamii inapowekeza katika malezi bora ya binti, inaweka msingi imara wa familia zenye ustawi na Taifa lenye maadili.
Mama bora haumbwi kwa bahati, bali hujengwa kupitia malezi yenye mwelekeo sahihi na endelevu.
