YANGA inadaiwa kufanya mazungumzo na winga wa Singida Black Stars, Lamin Jarjou kwa ajili ya kumsajili msimu ujao wa 2026/27 baada ya kuonyesha kiwango cha juu katika mechi za Ligi Kuu Bara msimu huu.
Jarjou ambaye anamuweka benchi Offen Chikola aliyejiunga na Singida BS kwa mkopo kutoka Yanga hadi sasa amefunga bao moja na asisti tatu, chanzo kilieleza mazungumzo yao yanakwenda vizuri na lolote linaweza kutokea.
Chanzo cha ndani kutoka Yanga kilisema: ”Yanga tuna timu nzuri, lakini lazima yatafanyika marekebisho kwa ajili ya msimu ujao. Jarjou ni kiungo mzuri ana kasi, anajua kudribo mipira, kwa kifupi ana kipaji cha juu.
Chanzo hicho kiliongeza: “Kila kitu kikikaa sawa tutafurahi kuona Jarjou anakuwa sehemu ya kikosi cha Yanga. Tunahitaji kuwa na timu bora na ushindani kila nafasi anayeingia na kutoka viwango visipishane.”
Endapo kama ishu hiyo itafanikiwa katika kikosi cha Yanga wanaocheza nafasi ya kiungo ni Mudathir Yahya mwenye mabao saba, Pacome Zouzoua ana matano, Maxi Nzengeli matatu na asisti tatu, Lassine Kouma bao moja, Duke Abuya asisti tano, hivyo Jarjou atakuwa na kazi ya kupambania namba.
“Tunahitaji timu ya kushindana na kikosi kipana kwa ajili ya ligi ya ndani na michuano ya kimataifa kwa msimu ujao,ndiyo maana tunazungumza na wachezaji mbalimbali pia kuna wengine wanaweza kuachwa,” kilisema chanzo hicho.
Mbali na Jarjou anayecheza pia kama kiungo mshambuliaji, pia kuna tetesi za Yanga kuhusishwa na mshambuliaji wa TRA, Ramadhan Chobwedo anayemaliza mkataba wake msimu huu, ambaye pia anahusishwa na watani zao, Simba.