Sowah afichua kinachoendelea Simba, klabu yatoa tamko

MSHAMBULIAJI wa Simba, Jonathan Sowah, amevunja ukimya na kuamua kuweka wazi kile kinachoendelea ndani ya klabu hiyo kumuhusu yeye ikiwa imepita takribani mwezi mmoja na siku 20 tangu asimamishwe klabuni hapo.

Februari 25, 2026 wakati Simba ikiwa Dodoma siku hiyo ikijiandaa kucheza dhidi ya Dodoma Jiji, zilitoka taarifa za Sowah kurudishwa Dar es Salaam kwa kile kilichodaiwa ni kuhitajika na Kamati ya Nidhamu ya klabu hiyo kujibu tuhuma zinazomkabili za utovu wa nidhamu.

Miongoni mwa kile kilichoelezwa anachotuhumiwa nacho Sowah hadi kufikia hatua ya kusimamishwa ni kuchelewa mazoezini huku akitakiwa kutoa maelezo ya kina, jambo ambalo alilifanya mbele ya kamati hiyo. Hata hivyo, siku chache mbele baada ya kujieleza, ziliibuka taarifa za mshambuliaji huyo raia wa Ghana kuandika barua ya kuvunja mkataba na Simba.

Kabla ya Sowah kusimamishwa na Simba, mshambuliaji huyo aliitumikia adhabu ya kukosa mechi tano kutokana na utovu wa nidhamu aliyopewa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) baada ya kikao chake cha Desemba 15, 2025. Adhabu hiyo ilimalizika Februari 25, 2026.

Akizungumza na Crown FM jijini Dar es Salaam, Sowah amesema mkataba wake na Simba bado upo hai, haujavunjika, huku akikiri kuitwa kwenye kamati ya nidhamu ya klabu hiyo na kufika kwenda kutoa maelezo kama alivyotakiwa.

Sowah aliyetua Simba dirisha kubwa la usajili msimu huu akitokea Singida Black Stars, amesema kwa sasa yupo Dar es Salaam, lakini hafanyi mazoezi na kikosi cha Simba.

“Ni nini ninachoweza kusema kuhusu utovu wa nidhamu?” Sowah alianza kwa kugusia utovu wa nidhamu anaotuhumiwa nao.

ADHA 03

“Unajua, binadamu tuna aina mbili au tuna aina tofauti za binadamu tulionao katika ulimwengu huu. Natumai unajua hilo. Hivyo hata wewe unayeniuliza una upande wako mzuri na una upande wako mbaya.

“Ikiwa mimi unaweza kusema ni mtaalamu, nikiwa mtaalamu, sina upande wangu mzuri, sina upande wangu mbaya? Moja kwa moja mimi ni binadamu, hivyo nitakuwa na mazuri na mabaya, sawa?

“Ikiwa nina mazuri na nina mabaya, je, umejiuliza ulinitendea nini ili mimi nibadilike na kuelekea upande wangu mbaya? Hivyo tunakubaliana kwamba inaweza kuwa kuna jambo fulani karibu nawe.”

Sowah ameendelea kwa kusema: “Watu hawataniwahi kunipata nikiwa huko nje na uniambie huyu hana nidhamu. Hapana. Wakati wowote utakaonipata kusema sina nidhamu ni uwanjani. Ndiyo maana nakuambia tuna aina mbili za binadamu; una upande wako mzuri na upande wako mbaya. Ninapocheza mpira na nikipoteza, nakasirika sana. Unanielewa?

“Wakati sifungi bao, nakasirika kwa sababu lengo langu ni kufunga bao, hivyo ikiwa sipati bao hilo, nahitaji kutafuta njia na namna ambayo inaweza kupata bao hilo; iwe nitapata bao na kupata kadi nyekundu, au nitapata bao na kupata kadi ya njano, sijali. Lengo langu ni kupata bao, ninataka kila wakati timu yangu iwe ya kwanza, huyo ndiye mimi.

“Mimi si mtu mchoyo, hivyo kila wakati watu walizoea kuona akiwa uwanjani hana heshima. Ndiyo, ni uwanjani tu ambapo unaweza kunipata. Watazame watu kama Balotelli (Mario), watazame watu kama Diego Costa… Watazame watu hawa leo wako wapi?”

Sowah ambaye huu ni msimu wake wa kwanza ndani ya Simba akiwa amefunga mabao matatu katika Ligi Kuu Bara, hakuishia hapo, ameendelea kwa kusema hajui ni nani anasambaza taarifa za kwamba yeye ni mtovu wa nidhamu.

“Kuhusu hilo, sijui kitu chochote, sijui kitu chochote. Sijui nani aliyeleta hizo habari. Unaelewa? Sijui kitu chochote kwa hiyo sitaki tu kulizungumzia.

“Kuhusu Simba, siwezi kuizungumzia Simba sasa hivi. Siwezi kuzungumza chochote kuhusu Simba.”

Nyota huyo ambaye msimu uliopita akiwa Singida Black Stars akicheza mechi 14 za Ligi Kuu Bara kwa takribani miezi sita akitua dirisha dogo na kufunga mabao 13, amesema: “Bado niko kwenye klabu (Simba). Nazungumza na wewe. Bado niko Tanzania.”

Kuhusu kuhudhuria kamati ya nidhamu na kilichojiri, Sowah alijibu kwamba alienda akisema: “Ndiyo, nilienda kule. Hicho ndicho ninachosema. Sitaki kuwazungumzia sasa hivi. Sitaki kuzungumza chochote kuhusu klabu kwa sasa.

“Mkataba wangu bado unafanya kazi. Kwa hiyo mimi ni mchezaji wa Simba. Sitaki tu kusema chochote kuhusu wao. Namaanisha bado niko Dar es Salaam.”

Alipoulizwa ishu za kuhudhuria mazoezi, amesema: “Hapana, hapana, hapana, hapana.”

Hata hivyo, Sowah amewatoa wasiwasi mashabiki wake akisema: “Hawapaswi kuwa na wasiwasi. Ndiyo maana wakati mwingine nahitaji kuja kwenye vyombo vya habari ili angalau nionekane kwao, nizungumze nao mara moja moja. Hapana, wasiwe na wasiwasi. Kila kitu kitakuwa sawa. Ninachoweza kusema ni kwamba nahitaji maombi yao na wanikumbuke kwenye maombi. Hivyo tu.”

ADHA 01

Tangu wakati huo wa sakata la Sowah na kusimamishwa kwake, Klabu ya Simba haikutoa tamko rasmi hadi leo Aprili 14, 2026 kupitia Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, aliposema: “Ni kweli Jonathan Sowah tulimsimamisha kutoka kwenye kambi yetu. Mwezi wa tatu tulisafiri kwenda Dodoma kucheza na Dodoma Jiji. Tukiwa pale tukiwa na Sowah akaamrishwa atoke kambini na kurejea Dar es Salaam.

“Sowah alikuwa akituhumiwa kwa makosa kadha wa kadha ya utovu wa nidhamu ambayo ni malalamiko yaliyokuja kutoka kwenye benchi la ufundi. Baada ya pale akarejeshwa kutoka Dodoma akarejea Dar es Salaam kusubiri taratibu za klabu ziweze kukamilika na hatimaye haki yake iweze kupatikana.

“Baada ya pale akawa amepelekwa kwenye kamati ya nidhamu ya Simba Sports Club ambayo inaongozwa na mwenyekiti wake, kamanda Kova (Suleiman), Sowah akaitwa mbele ya kamati akasomewa mashtaka yake yote ambayo yanamkabili na yapo ambayo amekiri na mengine yakatoa maelezo na baada ya pale kamati ikajiridhisha ya kwamba mchezaji huyu ana makosa ya utovu wa nidhamu. Baada ya kujiridhisha huko akapewa adhabu.”

ADHA 02

“Adhabu ya kwanza ni faini na adhabu ya pili ameamrishwa aende akafanye mazoezi na timu yetu ya vijana chini ya umri wa miaka 20. Adhabu hii inaanza mara moja kuanzia hivi sasa na atakuwa akifanya mazoezi na timu yetu ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ikiwa ni kipindi cha matazamio kumwangalia kama kutakuwa kuna mabadiliko yoyote ndani yake kwenye upande wa nidhamu basi adhabu yake hiyo itaisha na atarejea timu kubwa kwenda kuendelea na majukumu yake kama kawaida.

“Kwa hiyo huo ndio mustakabali wa Sowah na Simba Sports Club ya kwamba yupo kwenye kuitumikia adhabu yake aliyopewa ambayo ni kufanya mazoezi na timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ikiwa ni kipindi cha matazamio.”