ZAIDI zaidi ya 50 wenye umri chini ya miaka 18, wameshiriki katika mafunzo ya siku moja ya kikapu ya Mambo Youth Challenge, kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari ya Zanaki, jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Mratibu wa mafunzo hayo, Bahati Mgunda, yalifanyika Jumapili yakiwa na lengo la kuwakutanisha pamoja vijana na wengi wameyafurahia na kupenda kucheza mchezo huo, huku idadi kubwa wakijitokeza.
“Kama mafunzo yangefanyika Jumamosi, naamini idadi ingekuwa kubwa sana,” amesema Mgunda na kuwapongeza makocha waliojitokeza kutoa mafunzo hayo.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Fesali Shukuru anayeichezea Vijana ‘City Bulls’, aliwashukuru waandaaji kwa kuwapa mafunzo hayo, kwani yamemweka katika hali nzuri, akijiandaa na Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL) mwaka huu.
“Kwa kweli katika mafunzo haya, nimekutana na vijana wengi wanaocheza BDL ambao kwa kipindi kirefu hatujakutana nao,” amesema Shukuru.
Venance Kikusa wa Ukonga Kings amesema katika mafuzo hayo amejifunza mbinu nyingi za uchezaji.
“Nitatumia mbinu hizo nikiwa na timu yangu ya Ukonga Kings katika Ligi ya BDL mwaka huu,” amesema Kikusa.
