Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja linaendelea kuimarisha usalama wa raia na mali zao kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi.
Katika taarifa rasmi, Polisi wametoa ufafanuzi kuhusu tukio la kifo cha mwanamke raia wa Marekani lililotokea Aprili 8, 2026 majira ya saa 2:50 usiku katika Hoteli ya ZURI iliyopo Nungwi, Wilaya ya Kaskazini ‘A’, Unguja.
Mwanamke huyo ametambulika kwa jina la Ashly Jenae (maarufu kama Ashlee Jenae), mwenye umri wa miaka 31, ambaye alikuwa mshawishi (influencer) kwenye mitandao ya kijamii. Inadaiwa kuwa alijaribu kujidhuru akiwa ndani ya chumba namba 25 cha hoteli hiyo, kabla ya kuokolewa na kupelekwa katika hospitali binafsi ya North Valle, Nungwi.
Baadaye alihamishiwa katika Hospitali ya Ampolo, iliyopo Mjini Unguja, Mkoa wa Mjini Magharibi, ambapo alifariki dunia Aprili 9, 2026 majira ya saa 9:00 alasiri akiwa anaendelea kupatiwa matibabu.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, marehemu aliwasili Zanzibar Aprili 4, 2026 kwa ajili ya utalii akiwa na mwanaume aitwaye Joseph Issac McCann (45), ambaye inadaiwa kuwa ni mpenzi wake. Wawili hao walifikia awali katika Hoteli ya Kilindi kabla ya kuhamia Hoteli ya ZURI Aprili 6, 2026.
Taarifa zinaeleza kuwa kulikuwa na sintofahamu kati yao, hali iliyosababisha uongozi wa hoteli kuwatenganisha kwa kuwapatia vyumba tofauti kwa ajili ya usalama wao. Marehemu alibaki katika chumba namba 25 huku Joseph akihamishiwa chumba namba 65.
Hadi sasa, Joseph McCann anaendelea kuhojiwa na Jeshi la Polisi, huku hati yake ya kusafiria ikizuiliwa wakati uchunguzi ukiendelea. Polisi pia wanasubiri ripoti ya uchunguzi wa kitaalamu kutoka kwa madaktari ili kubaini chanzo halisi cha tukio hilo.
Jeshi la Polisi limewahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya usalama, na kutoa taarifa mapema wanapobaini viashiria vya hatari ili kuzuia matukio kama haya.
