RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya michezo ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyokubalika kimataifa.
Dk Mwinyi ameyasema hayo leo Aprili 14, 2026 alipotembelea mradi wa Mji wa Afcon (Afcon City) unaojengwa Fumba katika Mkoa wa Mjini Magharibi kisiwani Unguja.
“Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi hii ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyokubalika kimataifa,” amesema Dk Mwinyi.
Katika ziara hiyo, Dk Mwinyi amejionea hatua mbalimbali za ujenzi wa uwanja wa kisasa unaojengwa na Kampuni ya Orkum Group ya Uturuki ambao unatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya maandalizi ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2027.
Mashindano hayo yanatarajiwa kuanza Juni 19, 2027 hadi Julai 18, 2027 ambapo Tanzania, Kenya na Uganda zitashirikiana kuandaa fainali hizo, kwa Tanzania mechi zitachezwa Arusha, Dar es Salaam na Zanzibar.
Uwanja huo unaojengwa Fumba unakadiriwa kuchukua watazamaji 35,000 ukiwa na viwango vya ubora vinavyokubalika na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Aidha, Dk Mwinyi ametembelea na kukagua miundombinu inayotarajiwa kujengwa ikiwemo hospitali, barabara, migahawa, maduka makubwa pamoja na huduma nyingine zitakazouzunguka mji huo wa kisasa.
Amesema, maeneo hayo yatatumika kwa biashara na huduma nyingine zitakazochochea ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.
Naye, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Riziki Pembe Juma, amesema mradi wa Afcon unatarajiwa kugharimu dola za Marekani milioni 150 (zaidi ya Sh389.2 bilioni za Tanzania) ambao unalenga kuvutia watalii watakaofika kushuhudia mashindano hayo.
Kwa maana hiyo, Serikali inayatazamia mashindano hayo kuwa fursa ya kuitangaza Zanzibar na utalii.
