Watumishi sita kortini kwa tuhuma za kusababisha hasara ya Sh14 bilioni

Dar es Salaam. Watumishi sita wa Bohari ya Dawa (MSD) akiwemo mhasibu mwandamizi na wafamasia wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashtaka 37 yakiwemo ya wizi wa dawa na vifaatiba vyenye thamani ya Sh5.537 bilioni, mali ya MSD.

Pia, washtakiwa hao kwa makusudi wanadaiwa kuisababishia MSD hasara ya Sh14.6 bilioni.

Washtakiwa katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 7833 ni Mhasibu Mwandamizi, Suddi Abas (34), mkazi wa Kibamba Shule.

Wengine ambao wote ni wafamasia ni Petro Mdegela (42), mkazi wa Manga Veta; Rashid Hassan (34) na mkazi wa Isyesye mkoani Mbeya.

Pia yupo, Edward Tengulaga (40), mkazi wa Manga Veta Mbeya na Mfamasia wa Halmashauri ya Wilaya ya Momba mkoani Songwe, Jackson Mahagi (39) ni mfamasia wa Halmashauri ya Wilaya ya Momba na Wema Mohamed (39) ambaye ni mfamasia wa Wilaya ya Singida na mkazi wa Mandewa.

Watumishi hao wanadaiwa pia kutakatisha fedha kiasi cha Sh5.537 bilioni kwa kununua mashamba, viwanja, gari, kujenga nyumba za kuishi na zingine za kupangisha, kuanzisha kampuni ya usafirishaji, kufungua duka la vifaa ya ujenzi pamoja na kufungua maduka ya dawa.

Washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo jana jioni Jumatatu Aprili 13, 2026 na kusomewa mashtaka yanayowakabili na wakili wa Serikali Mwandamizi, Clara Chame, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya.

Hata hivyo, kabla ya kusomewa mashtaka hayo, Hakimu Lyamuya aliwaeleza washtakiwa hao hawatakiwi kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi isipokuwa kwa kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP).

Vilevile, shtaka la kutakatisha fedha linalowakabili, halina dhamana hivyo wataendelea kusabaki rumande.

Hakimu Lyamuya baada ya kueleza hayo, Wakili Chame aliwasomea mashtaka yao.

Kati ya mashtaka 37 yanayowakabili washtakiwa hao, mashtaka 31 ni ya kutakatisha fedha; matatu ni ya wizi wakiwa watumishi; mawili ni kuisababishia mamlaka hasara na moja ni kuongoza genge la uhalifu.

Wakili Chame alidai shtaka la kwanza ni kuongoza genge, ambapo washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kati ya Julai Mosi, 2021 na Juni 30, 2025 katika maeneo tofauti ya Mkoa wa Dar es Salaam, Mbeya, Songwe, Dodoma, Singida na maeneo mengi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa makusudi waliongoza genge la uhalifu kwa kutenda kosa la wizi wakiwa watumishi

Shtaka la pili ni wizi wakiwa watumishi, linalomkabili Abas, Mdegela, Hassan na Tengulaga, ambapo wanadaiwa kati ya Julai Mosi, 2021 na Juni 30, 2025 katika maeneo tofauti ya mkoa wa Dar es Salaam na Mbeya, wakiwa watumushi kwa vyeo vyao, wanadaiwa kuiba dawa na vifaatiba yenye thamani ya Sh2.695 bilioni, mali ya MSD, iliyofika mikononi mwao wakiwa waajiriwa.

Shtaka la tatu ni wizi linalowakabili mshtakiwa Abasi, Mdegela, Hassan na Mahagi, siku na maeneo hayo, washtakiwa wanadaiwa kuiba Sh2.592 bilioni, mali ya MSD iliyofika mikononi mwao wakiwa waajiriwa.

Shtaka la nne ni wizi wakiwa watumishi wa MSD linalomkabili Abas na Mohamed, ambapo wanadaiwa kati ya Januari 1, 2023 na Juni 30, 2025 katika maeneo tofauti ya Dar es Salaam, Dodoma na Singida, kwa pamoja wanadaiwa kuiba Sh250 milioni, mali ya MSD.

Iliendelea kudaiwa mahakamani hapo, kuwa shtaka la tano ni kuisababishia mamlaka hasara, shtaka linalomkabili Abas pekee yake, ambapo anadaiwa katika tarehe hizo, ofisi za MSD zilizopo Keko, Wilaya ya Temeke, mshtakiwa kwa makusudi aliisababishia MSD hasara ya Sh9.1 bilioni.

Shtaka la tano ni kuisababishia mamlaka hiyo hasara linalowakabili washtakiwa wote, ambapo katika kipindi hicho na katika mikoa hiyo, washtakiwa waliisababishia MSD hasara ya Sh5.537 bilioni.

Shtaka la saba ni kutakatisha fedha, linalowakabili washtakiwa wote, ambapo katika kipindi hicho, wanadaiwa kutakatisha fedha kiasi cha Sh5.537 bilioni huku wakijua shtaka hilo ni zao la kosa tangulizi la wizi wakiwa watumishi.

Shtaka la 8 hadi 10 ni la kutakatisha fedha na linamkabili Tengulaga pekee yake, ambapo anadaiwa kati ya Januari 2021 na Aprili 2025 eneo la Sinjilili, Wilaya ya Chunya, mshtakiwa kwa lengo la kuficha uhalali wa fedha Sh2.695 bilioni, alinunua kiwanja eneo hilo na kujenga nyumba nane (tatu ni za kuishi zilizopo eneo la Manga Veta Mbeya na tano ni za kupangisha (Apartment) zilizopo Chunya, wakati akijua fedha hizo ni zao la kosa tangulizi la wizi akiwa mwajiriwa.

Shtaka la 11 hadi 20 ni la kutakatisha fedha linalomkabili Mdegela ambapo kati ya Julai 1, 2021 na Juni 2025 eneo la Mwansekwa Manga Veta mkoani Mbeya, kwa lengo la kuficha asili au uhalali wa Sh2.695 bilioni na Sh5.537bilioni, mshtakiwa alijenga nyumba za kuishi, zilizopo eneo la Manga Veta mkoani Mbeya.

Vilevile Mdegela anadaiwa kununua viwanja saba; kufungua kampuni ya usafirisha yenye jina la Zenati Investment Limited pamoja na kufungua duka la vifaa vya ujenzi mkoani humo, wakati akijua fedha hizo ni zao la kosa tangulizi la wizi akiwa mwajiriwa.

Shtaka la 21 hadi 25 ni la kutakatisha fedha linalomkabili mshtakiwa Mahagi, ambaye anadaiwa katika tarehe hizo, maeneo ya Manga Veta na Mwansekwa yaliyopo mkoa wa Mbeya na maeneo ya Mlowo na Nyiimbiri Lukutululi (Mkoa wa Songwe), Mahagi akiwa Mfamasia wa Halmashauri ya Mombo, kwa lengo la kuficha asili na uhalali wa fedha kiasi cha Sh5.595 bilioni, alinunua viwanja na mashamba, ambapo ekari nne alipanda miti ya mbao eneo la Vwawa.

Pia, Mahagi anadaiwa kutumia fedha hizo kujenga nyumba eneo la Manga Veta na kufungua duka la dawa na lenye jina la Mseke Pharmacy lililopo eneo la Soweto, wakati akijua fedha hizo ni zao la kosa tangulizi la wizi akiwa mtumishi.

Kuanzia shtaka la 25 hadi 37 ni ya utakatishaji fedha na yanamkabilili Mohamed pekee yake, ambapo katika tarehe hizo mkoani Singida, Dar es Salaam, Dodoma na Pwani, Mohamed akiwa Mfamasia wa Wilaya ya Singida, kwa lengo la kuficha asili na uhalali wa fedha kiasi cha Sh250 milioni, aliamua kujenga nyumba tatu zilizopo Singida.

Pia, alinunua viwanja vitatu vilivyopo Ilazo (Dodoma) Kijitonyama kwa Ally Maua (Kinondoni) na Kibada (Kigamboni).

Vilevile Mohamed anadaiwa kununua gari tatu aina ya toyota IST, Premio na Audi.

Mohamed anadaiwa pia kufungua maduka matatu ya dawa za binadamu nyenye jina la Setif Pharmacy (Singida), Vagas Pharmacy (Singida) na Mig Pharmacy lilliopo Gongo la Mboto (Dar es Salaam), huku akijua hizo ni zao la kosa tangulizi la wizi akiwa mtumishi.

Upande wa Jamhuri baada ya kumaliza kuwasomea mashtaka yao, ulidai kuwa upelelezi haijakamilika na kwamba wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Mshtakiwa wanatetewa na mawakili Method Kagoma, Raymond Swai, Musa Mhagama na Seif Wembe.

Hakimu Lyamuya aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 27, 2026 itakapotajwa.

Washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na mashtaka ya kutatisha fedha yanayowakabili hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.