Wapangaji wa NHC wapinga kupewa notisi ya siku 90 kupisha mradi

Arusha. Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limewapa notisi ya siku 90 wapangaji wake wanaoishi na kufanya biashara katika nyumba zake zilizopo mitaa ya Nyamezi na Sokoine, jijini hapa, ili kupisha mpango wa uendelezaji wa majengo ya kisasa.

Hata hivyo, hatua hiyo imeibua upinzani kutoka kwa wapangaji hao, ambao wameeleza kuwa muda waliopangiwa ni mfupi ukilinganishwa na hali halisi ya maisha na biashara zao.

Wakizungumza na Mwananchi kwa sharti la kutotajwa majina yao, baadhi ya wapangaji wamesema wamekuwa wakiishi na kufanya biashara katika eneo hilo kwa muda mrefu, wengine zaidi ya miongo minne, hivyo wanahitaji muda wa kutosha kujiandaa kuhama.

“Tumekuwepo hapa kwa zaidi ya miaka 40. Siku 90 hazitoshi kabisa kupata sehemu mbadala ya biashara na makazi. Tunaomba tupewe angalau miezi 18 ili tuweze kujipanga vizuri,” amesema mmoja wa wapangaji hao.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana, eneo linalotarajiwa kuendelezwa lina jumla ya maduka makubwa 40 pamoja na makazi ya familia 50, likiwa katikati ya Jiji la Arusha.

Notisi iliyotolewa na NHC imeanza kutumika Aprili 1 na inatarajiwa kumalizika Juni 30 mwaka huu, ambapo wapangaji wote wanapaswa kuwa wamehama ifikapo mwisho wa muda huo.

Wapangaji hao wameiomba NHC kuzingatia athari za kijamii na kiuchumi zinazoweza kujitokeza kutokana na uamuzi huo, ikiwamo kupoteza wateja, ajira na changamoto za kupata maeneo mbadala ndani ya muda mfupi.

Sehemu ya nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) mtaa wa Sokoine jijini Arusha ambazo wapangaji wake wamepewa notisi ya siku 90 kupisha mradi wa maendelezo. Picha na Filbert Rweyemamu

“Wapangaji tupo tayari kuhama lakini muda tuliopewa ni mdogo ukizingatia muda tuliokaa kwenye hizi nyumba, tupo tayari kuheshimu sheria ya upangishaji lakini NHC iangalie njia sahihi inayozingatia utu katika kipindi hiki kifupi siyo rahisi kupata nyumba za biashara na makazi tunaomba tupewe muda zaidi,”wamesema wapangaji hao.

Hata hivyo, mmoja wa wapangaji mwenye duka la bidhaa mbalimbali amesema biashara anayoifanya amekopa akitarajia kuwarejeshea waliompa bidhaa kwa njia ya kuziuza na iwapo watalazimika kuhama kutatokea changamoto ya kufikia malengo na wale aliowakopesha bidhaa watashindwa kumlipa jambo litakalomsababishia hasara.

Meneja wa NHC Mkoa wa Arusha, Nistas Mvungi, alipotafutwa kwa ufafanuzi alisema mamlaka ya kuzungumzia mradi wa uendelezaji wa eneo hilo, unaotarajiwa kuwa na manufaa kwa wapangaji, ipo makao makuu ya shirika hilo.

Kwa upande wake, Meneja wa Habari na Uhusiano wa NHC, Muungano Saguya, amesema mradi unaotarajiwa kujengwa katika eneo hilo utakuwa na manufaa makubwa, kwani unalenga kuleta maendeleo ya kisasa yanayoendana na kasi ya ukuaji na hadhi ya Jiji la Arusha kwa sasa na katika miaka ijayo.

Amesema maendeleo yanayotekelezwa na shirika hilo yanalenga kuboresha mazingira ya wapangaji katika kuendesha biashara zao, na kwamba mradi utakapokamilika, wanufaika wa kwanza watakuwa ni wapangaji waliopo kwa sasa.

 “Shirika la Nyumba la Taifa linapotaka kufanya uendelezaji wa eneo kwenye majengo yake yeyote iwe Arusha, Dodoma, Dar es Salaam au mkoa wowote notisi inayotakiwa kutolewa kwa mujibu wa sheria namba nne ya mwaka 1999 ni notisi ya siku 30, sasa tunapotoa siku 90 ni kibinadamu ili kuwapa muda wa kutosha ili kutafuta eneo jingine la biashara na makazi,” amesema Saguya.

Amesema kuwa licha ya mikataba iliyopo kati ya NHC na wapangaji, shirika linao uwezo wa kusitisha mikataba hiyo pindi inapoona inafaa kulingana na mazingira yaliyopo na kuwa sababu za NHC kusitisha mikataba hiyo zina maslahi mapana ya maendelezo.

Saguya amesema mradi huo utakapokamilika utachukua watu wengi ukilinganisha na waliopo sasa hivi pia utaongeza unadhifu na mwonekano wa Jiji la Arusha ambalo lina ofisi mbalimbali za kanda,kitaifa na kimataifa.