Dar es Salaam. Serikali imeibua pingamizi la awali dhidi ya kesi ya mawakili wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, anayeshikiliwa katika mahabusu ya Gereza la Ukonga, Dar es Salaam, kutokana na kukabiliwa na kesi ya uhaini.
Kesi hiyo ya kikatiba namba 7300/2026 imefunguliwa Mahakama Kuu, Masjala Kuu ya Dodoma, na mawakili watatu— Kulwa Maduhu, Nashon Nkungu na Paul Kisabo, wakipinga vikwazo wanavyowekewa na Mkuu wa Gereza la Ukonga kila wanapokwenda gerezani kuzungumza na mteja wao, Lissu.
Mawakili hao wamefungua kesi hiyo dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Kamishna Mkuu wa Magereza (CGP), Mkuu wa Gereza la Ukonga, jijini Dar es Salaam na Lissu mwenyewe.
Hata hivyo, Serikali kupitia AG, ambaye ni mdaiwa wa kwanza katika kesi hiyo, imewawekea kigingi baada ya kuibua pingamizi la awali ikiomba mahakama hiyo iitupilie mbali kesi hiyo bila hata kuisikiliza, hasa madai ya msingi ya mawakili hao.
Pingamizi hilo limebainishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Vivian Method, akisaidiwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Stanley Kalokola, wakati kesi hiyo ilipotajwa kwa mara ya kwanza leo, kwa njia ya mtandao (video conference).
Kesi hiyo inasikilizwa na jopo la majaji watatu— Amir Mruma (kiongozi wa jopo), Dk Angelo Rumisha na Dk Everist Longopa.
Kwa mujibu wa notisi ya pingamizi hilo ambayo Mwananchi limeiona nakala yake, Serikali imesema kuwa katika tarehe ya usikilizwaji wa kesi hiyo itaibua pingamizi la awali na kuiomba mahakama iitupilie mbali kesi hiyo.
Notisi hiyo imebainisha sababu moja ikidai kuwa mahakama haipaswi kuisikiliza kesi hiyo kwa kuwa haikubaliki kisheria na ni batili.
“Kesi hii haiwezi kusikilizwa na ni batili kisheria, kwa kuwa wadaiwa wana njia mbadala za kupata nafuu (wanazoziomba), hivyo inakiuka masharti ya kifungu cha 8(2) cha Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi na Wajibu (Sura ya 3, Marejeo ya 2023),” inasomeka notisi hiyo.
Hivyo, mahakama italazimika kusikiliza kwanza na kulitolea uamuzi pingamizi hilo, na hatima ya kuendelea na usikilizwaji wa kesi hiyo itategemea uamuzi wa pingamizi hilo, iwapo wadai watavuka kigingi hicho cha pingamizi la Serikali.
Pia, Wakili Method ameieleza mahakama kuwa wameshawapatia wahusika nyaraka za kesi hiyo, yakiwemo majibu ya madai na taarifa hiyo ya pingamizi, isipokuwa mdaiwa wa nne, Lissu.
Wakili wa wadai katika kesi hiyo, John Seka, ameithibitishia mahakama kupokea majibu ya pamoja ya wadaiwa wa kwanza mpaka wa tatu (AG, CGP na Mkuu wa Gereza la Ukonga), pamoja na taarifa ya pingamizi.
Kutokana na hali hiyo, Jaji Mruma ameelekeza Lissu apewe majibu ya Serikali na notisi ya pingamizi ili naye ajue kile ambacho wadaiwa hao wamekieleza.
Lissu ameiomba mahakama iizingatie kuwa yuko mahabusu na kwamba katika kuwasilisha majibu yake atahitaji kukutana na wakili wake kwa ajili ya kumuapisha wakati atakapoandaa majibu yake na kiapo kinzani, huku akipendekeza muda wa wiki tatu.
Mahakama imepanga kesi hiyo itajwe tena Mei 5, 2026, kwa ajili ya kuangalia kama taratibu za ubadilishanaji nyaraka za kesi hiyo zimekamilika na kwa ajili ya maelekezo mengine.
Wadai wanajitambulisha kuwa washauri wa kisheria wa Lissu, wakilalamikia matendo ya mdaiwa wa tatu (Mkuu wa Gereza la Ukonga) kushindwa kutekeleza Kanuni ya 13 ya Kanuni za Magereza inayotoa haki ya washauri wa kisheria kufanya mashauriano ya siri na wateja wao bila kuingiliwa.
Maduhu akidai kuwa kati ya Septemba 2025 na Machi 2026 amekuwa akizuiliwa na maofisa magereza kukutana na kushauriana na Lissu au kumpelekea nyaraka muhimu zinazohusiana na kesi inayomkabili, huku Mkuu wa Gereza akimweleza kuwa anatekeleza maagizo ya Kamishna Mkuu wa Magereza.
Kwa upande wake, Nkungu na Kisabo, licha ya kupata fursa ya kuzungumza na kujadiliana na Lissu masuala ya kisheria, wamekuwa hawana faragha kwani maofisa magereza wamekuwa wakisimama umbali wanaoweza kusikia kila kitu wanachojadiliana.
Pamoja na nafuu nyingine, wanaiomba mahakama itamke kuwa maofisa magereza kusikiliza mazungumzo na mteja wao, Lissu, ni kinyume cha Kanuni ya 13 ya Kanuni za Magereza, sheria na Katiba kuhusu haki ya kusikilizwa kwa usawa na faragha.
Pia, wanaomba amri ya mahakama, wakati kesi hiyo ikisubiri kusikilizwa na kuamuriwa, wapewe haki ya kushauriana na mteja wao, Lissu, kwa faragha.
