Dk Mwinyi akagua Mji wa Afcon Zanzibar, aahidi viwango vya kimataifa

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya michezo ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyokubalika kimataifa.

Dk Mwinyi ameyasema hayo leo Jumatatu Aprili 14, 2026 wakati akitembelea mradi wa Mji wa Afcon (Afcon City) unaojengwa Fumba, Mkoa wa Mjini Magharibi.

“Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi hii ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyokubalika kimataifa,” amesema.

Ujenzi wa mradi wa Mji wa AFCON Fumba uliopo Mkoa wa Mjini Magharibi.

Katika ziara hiyo, amejionea hatua mbalimbali za ujenzi wa uwanja wa kisasa unaojengwa na kampuni ya Orkum Group ya Uturuki ambao unatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya maandalizi ya fainali za kombe la mataifa ya Afrika (Afcon).

Mashindano hayo yanatarajiwa kuanza Juni 19 hadi Julai 18,  ambapo Kenya, Uganda na Tanzania zitashirikiana kuandaa fainali hizo, kwa Tanzania mechi zitachezwa Arusha, Dar es Salaam na Zanzibar.

Uwanja huo unaojengwa Fumba unakadiriwa kuwa na uwezo wa kuchukua watazamaji 35,000 ukiwa na viwango vya ubora vinavyokubalika na Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF).

Aidha, Rais Dk Mwinyi ametembelea na kukagua miundombinu inayotarajiwa kujengwa ikiwemo hospitali, barabara, migahawa, maduka makubwa pamoja na huduma nyingine zitakazozunguka mji huo wa kisasa.

Amesema maeneo hayo yatatumika kwa biashara na huduma nyingine zitakazochochea ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.

Naye, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Riziki Pembe Juma amesema mradi wa Afcon unatarajiwa kugharimu Dola za Marekani 150 milioni sawa na Sh388.8 bilioni ambao unalenga kuvutia watalii watakaofika kushuhudia mashindano hayo.

Hivyo, Serikali inayatazamia mashindano hayo kuwa fursa ya kuitangaza Zanzibar na utalii.