Bodaboda wawili wafariki dunia kwa kuigonga treni, Tabora

Tabora. Madereva bodaboda wawili mjini Tabora wamefariki dunia baada ya kuigonga treni katika makutano ya reli na barabara katika Kata ya Malolo, Manispaa ya Tabora mkoani Tabora.

Hayo yamebainishwa leo Aprili 14, 2026 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ajali hiyo.

Amesema ajali hiyo imehusisha treni ya abiria iliyokuwa ikitoka Tabora kwenda Kigoma ambapo iligongwa na waendesha bodaboda katika kivuko cha reli na barabara maeneo ya Malolo, Manispaa ya Tabora.

“Njia ya treni lazima uizingatiwe kabla ya kuvuka au kufanya jambo lolote kwa sababu treni haiwezi kupisha, hivyo unapoingia kwenye njia yake haiwezi kufunga breki au kukupisha,” amesema.

Amesema chanzo cha ajali hiyo ni madereva hao wa bodaboda kutochukua tahadhari kwenye njia ya treni kama ambavyo sheria inamtaka mtumiaji wa barabara kuheshimu vivuko hivyo.

“Unapokuwa unatumia barabara lazima uzingatie pia sheria za usalama barabarani ili kuepusha kugharimu maisha pamoja na usumbufu kwa watumiaji wengine wa barabara,” amesema.

Kamanda Abwao ametoa wito kwa watumiaji wote wa barabara kuhakikisha wanachukua tahadhari kwa sababu treni haiwezi kupisha kitu kilichoingia kwenye njia yake.

Mwenyekiti wa waendesha bodaboda Wilaya ya Tabora, Michael Mtuve amewataja waliofariki ni Ramadhani Yasini, mkazi wa Malolo aliyekuwa akifanya shughuli zake mjini kati Tabora, mwingine hajafahamika mpaka sasa lakini juhudi za kumtambua zinaendelea.

Mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo, Mwajuma Nkulu amesema bodaboda hao waliokuwa watatu walikuwa mwendokasi sana, wa kwanza alifanikiwa kupita na hao wengine wawili ndio wakagonga hiyo treni.

“Yaani walikuwa wanakimbia sana wamefuatana kama wanashindana vile, yule mmoja kapita mbio, hawa wawili wakajaa kwenye treni, wakafariki palepale, ndipo wakaja watu wa Zimamoto wakachukua ile miili yao,” amesema.

Shuhuda mwingine, Juma Shilaja amesema wakati treni inakuja ili ivuke, alishangaa kuona hao bodaboda wamejigonga kwenye treni na baada ya kusogea akakuta tayari wamepoteza maisha kutokana na vile walivyokuwa wamepata majeraha.

“Kiukweli, hivi vivuko vya treni na barabara Tabora hatuwezi kulaumu tena Serikali kwa sababu alama zimewekwa na zile ishara za kujulisha kama treni inakuja, zipo. Ni sisi tu na uzembe wetu au ndio siku ya kufa imefika,” amesema.