Dar es Salaam. Jumla ya Sh13.7 trilioni zimetolewa na Benki ya CRDB kwa ajili ya kukuza uchumi wa Afrika Mashariki na Kati katika sekta za biashara, viwanda, miundombinu na biashara ndogo na za kati (SMEs).
Hayo yamebainishwa katika matokeo ya fedha yaliyokaguliwa na kutangazwa leo, Jumanne Aprili 14, 2026, na CRDB.
Kwa mujibu wa CRDB, ukuaji huo unaonesha mchango wa taasisi hiyo katika uchumi wa kikanda kwenye utoaji wa huduma za kifedha.
Pia, hatua hiyo imeifanya CRDB kuwa mdau muhimu katika kusaidia ukuaji wa sekta za biashara, kilimo, nishati, usafirishaji na maendeleo ya wajasiriamali Tanzania, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kanda hiyo.
“Lengo letu si tu kukua, bali kuhakikisha ukuaji huo unaleta matokeo chanya katika uchumi. Tunachukua hatua mahsusi kuelekeza mitaji katika sekta zinazochochea ajira, kurahisisha biashara na kuimarisha ustahimilivu wa uchumi wetu,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Abdulmajid Nsekela.
Kukua kwa mchango wa CRDB katika uchumi wa Afrika Mashariki kunatokana na matokeo mazuri ya kifedha kwa mwaka 2025, ambapo jumla ya mali iliongezeka kwa asilimia 33.6 kufikia Sh22.3 trilioni.
Pia, amana za wateja zimekua kwa asilimia 36.1 hadi Sh14.7 trilioni, zikiimarisha msingi wa ukwasi kwa ajili ya upanuzi endelevu.
Kwa mara ya kwanza CRDB imerekodi faida kabla ya kodi ya zaidi ya Sh1 trilioni, huku faida baada ya kodi ikiongezeka kwa asilimia 32.1 kufikia Sh728.6 bilioni, wakati mtaji wa wanahisa ulifikia Sh2.78 trilioni.
“Matokeo haya yanaimarisha mchango wa benki hiyo katika uchumi halisi, ikihama kutoka mafanikio ya kifedha pekee kwenda kwenye athari inayoonekana. Kukua huko kwa faida kumechangiwa na ongezeko la mapato yatokanayo na riba pamoja na ukuaji wa mapato yasiyotokana na riba, hususan ada na kamisheni, ambapo jumla ya mapato ya uendeshaji yalifikia Sh1.03 trilioni,” amesema Nsekela.
Nsekela amesema hatua hiyo inaakisi ongezeko la miamala, matumizi ya huduma za kidijitali na uhusiano mpana zaidi na wateja katika masoko mbalimbali.
Amefafanua kuwa zaidi ya viashiria hivyo vya kifedha, CRDB inaendeleza ajenda yake ya kukuza ujumuishi wa kifedha kupitia mtandao wake wa utoaji huduma unaojumuisha kampuni zake tanzu za CRDB Foundation na CRDB Insurance.
“Dhamira yetu ni kuchochea na kukuza ujumuishi wa kifedha na kiuchumi. Kipaumbele chetu ni kuhakikisha mitaji inafika maeneo yanayofungua fursa, kusaidia maisha ya watu na kuwezesha maendeleo endelevu,” ameeleza.
Ofisa Mkuu wa Fedha, Frederick Nshekanabo, amesema misingi imara ya benki inaendelea kuimarisha faida na uendelevu wake.
“Uwiano wetu wa faida kwa mtaji wa wanahisa wa asilimia 29.5 unaonesha uwezo wetu wa kuzalisha thamani kubwa kwa wanahisa huku tukiendelea kuwekeza kwa ajili ya ukuaji. Zaidi ya asilimia 84 ya mali zetu zinazalisha mapato, jambo linaloashiria ufanisi na uendelevu wa muda mrefu,” amesema.
