Simulizi ya Mwakalindile aliyepata ulemavu wa kudumu

Mbeya. Mkazi wa Mtaa wa Igamba, Kata ya Nsalaga, Uyole, Philipo Mwakalindile (54), amejikuta akipitia vipindi vigumu vya namna ya kuendesha maisha ya kila siku baada ya kupata ulemavu wa kudumu katika mkono wake wa kushoto.

Mwakalindile, ambaye licha ya kupata ulemavu wa kudumu ametengwa na familia yake, jambo ambalo limemfanya kuishi maisha ya tabu na kuomba misaada ya chakula na mahitaji mengine kwa majirani.

Mbali na kukosa mahitaji, amekuwa akiishi kwenye nyumba hatarishi iliyojengwa kwa tofali za tope huku ikiwa na tundu kubwa kwenye lango kuu la kuingia ndani.

Kufuatia changamoto hizo, Spika wa Bunge mstaafu na Mbunge wa Uyole amebeba jukumu la kubomoa makazi yake ya awali na kumjengea nyumba bora ya kisasa.

Muonekano wa eneo la miundombinu ya choo cha  Philipo Mwakalindile (54),kikiwa katika halo mbaya na kutitia kufuatia kunyonya maji ya mvua na kuwa katika hatari ya kubomoka.Picha na Hawa Mathias

Hatua hiyo imekuja ikiwa zimepita siku kadhaa baada ya mbio za Bendera ya Upendo kumuibua na kushirikisha viongozi wa Serikali ya Mtaa wa Igamba kwa ajili ya hatua za kuanza ujenzi rasmi.

Leo Aprili 14, 2026, Taasisi ya Tulia Trust imeanza rasmi ujenzi wa nyumba hiyo huku wananchi wakijitoa kushiriki nguvu kazi ili kuhakikisha inakamilika ndani ya mwezi mmoja.

Awali, akizungumza na Mwananchi Digital leo, Mwakalindile ameeleza magumu na machungu anayopitia baada ya familia yake kumtenga.

Anasema mwaka 2016 alipata ajali ya gari wakati wakisafirisha msiba kutoka Mbeya kwenda Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya.

“Tukiwa tumepanda kwenye gari la wazi kusafirisha msiba, tulipita eneo lenye miti mikubwa mingi, lakini wenzangu waliinama, mimi sikuona ndipo tawi lilinipiga kwenye mkono wa kushoto na kusababisha ulemavu wa kudumu,” amesema.

Amesema baada ya kupata ulemavu imekuwa mwiba kwake kwani familia ilimtelekeza na kukosa msaada wa matibabu mpaka kufikia hali hiyo ya kuishi kwa kukosa usaidizi.

“Kimsingi nashindwa kusema lolote maana bado nina maumivu makali sana. Hapa naishi peke yangu na wapangaji wawili tu ambao kwa namna moja au nyingine wamekuwa msaada wangu,” amesema.

Amesema kutokana na magumu na visa mikasa anavyopitia, anashukuru Taasisi ya Tulia Trust kwa msaada wa kuanza ujenzi wa makazi yake, jambo ambalo litarejesha tabasamu lililopotea.

“Sasa naona matumaini mapya ya maisha, lakini pia niombe msaada wa kupata mtaji wa biashara ya kujumuia zao la mpunga Wilaya ya Mbarali ili kujikwamua kiuchumi,” amesema.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi vifaa vya ujenzi wa nyumba hiyo, mwakilishi wa taasisi hiyo, Hady Kalinjila, amesema hatua hiyo ni baada ya kubaini mazingira magumu na hatarishi ya makazi ya Mzee Mwakalindile.

Nyumba ya awali aliyokuwa akiishi Philipo Mwakalindile (54),kabla ya Taasisi ya Tulia Trust kuboa kwa ajili ya kujenga nyumba ya kisasa katika Mtaa wa Igamba Kata ya Nsalaga Halmashauri ya Jiji la Mbeya. Picha na Hawa Mathias

“Awali tulibaini mazingira magumu ya maisha yake, lakini pia nyumba yake ilikuwa mbovu ya tope, ndipo tulitoa taarifa kwa Mkurugenzi wa Taasisi, Dk. Tulia, ambaye alitoa maelekezo kwa ajili ya kuanza ujenzi huo,” amesema.

Katika hatua nyingine, Kalinjila ameomba wananchi kutoa ushirikiano hatua kwa hatua ili kukamilisha ujenzi wa nyumba hiyo ndani ya siku 30.

“Wakati tunaanza ujenzi, tunamshukuru Diwani wa Kata ya Nsalaga, Clement Mwandemba, kwa kumpangia nyumba ya kumstiri mhitaji,” amesema.

Mkazi wa Mtaa wa Igamba, Janeth Solomon, amesema kimsingi mazingira ya maisha ya Mwakalindile ni magumu na yanahitaji msaada wa karibu.

“Huyu mzee tangu apate ulemavu, familia yake imemtelekeza. Amekuwa akiishi maisha ya tabu na kukosa msaada, ikiwemo chakula na mahitaji mengine,” amesema.

Diwani wa Kata ya Nsalaga, Clement Mwandemba, amesema ataungana na vijana wa taasisi hiyo kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati.

“Kimsingi nimshukuru sana Mbunge wa Uyole kwa kujitokeza kujenga makazi ya mhitaji huyu ambaye anapitia vipindi vigumu vya kuendesha maisha ya kila siku,” amesema.