Mtendaji wa kijiji kizimbani kwa tuhuma za rushwa

Hanang. Ofisa Mtendaji wa Kijiji (VEO) cha Qutesh kilichopo Wilaya ya Hanang mkoani Manyara, Senesa Gidang’adi amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya, akisomewa shtaka la rushwa.

Gidang’adi amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Hanang na kusomewa shtaka la uhujumu uchumi Aprili 13, 2026 katika shauri namba 7732/2026.

Mbele ya hakimu mkazi wa Mahakama ya wilaya hiyo, Pollena Ilon, mtendaji huyo ameshtakiwa kwa kosa la ufujaji, ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka akiwa mtumishi wa umma.

Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Wilaya ya Hanang, Daudi Kingazi amesema mshtakiwa huyo ametenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 28 (1) na 31 vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, sura ya 329 R.E 2023.

Kingazi ameieleza Mahakama hiyo kuwa mshtakiwa alitumia madaraka yake vibaya kwa kufanya ubadhirifu wa Sh800,000 za kukodisha mashamba.

Amesema mtuhumiwa huyo hakufikisha fedha hizo katika akaunti ya kijiji hicho, kinyume na kifungu cha 50 (5) cha Sheria ya Uhifadhi wa Fedha za Serikali za Mitaa ya mwaka 2009.

Hata hivyo, mshtakiwa huyo amekana kufanya kosa hilo mahakamani hapo mara baada ya hakimu kumuuliza endapo ni kweli amefanya kosa hilo.

Mshtakiwa huyo yupo nje kwa dhamana ya Sh2 milioni na mdhamini mmoja mwenye utambukisho wa barua kutoka serikali ya mtaa.

Hakimu Iloni ameiahirisha kesi hiyo hadi Mei 5, 2026 itakaposomewa maelezo ya awali (PH).