Dar es Salaam. Wakati idadi ya watoto wanaokabiliwa na matatizo ya mfumo wa fahamu ikiendelea kuongezeka nchini, imebainika kuna madaktari bingwa watatu pekee wa ubongo kwa watoto wanaohudumia maelfu ya wagonjwa, hali inayotia shaka upatikanaji wa huduma bora za afya kwa kundi hilo nyeti.
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, inaonesha kuwa kati ya idadi ya watoto 40,166 waliobainika kuwa na matatizo ya mfumo wa fahamu katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Rukwa na Tabora, kulikuwa na madaktari bingwa wawili pekee.
Licha ya kuwepo kwa zaidi ya watoto 11,600 wenye kifafa na wengine zaidi ya 11,300 wenye ulemavu wa ubongo katika Jiji la Dar es Salaam pekee, bado wataalamu waliopo ni wachache kulinganisha na mahitaji halisi.
Hayo yamebainishwa kupitia Ripoti ya Ukaguzi wa Utendaji Kuhusu Utoaji wa Huduma za Afya ya Mfumo wa Fahamu kwa Watoto na Ripoti Kuu ya Mwaka ya Ufanisi kwa mwaka 2024/2025, zilizowasilishwa bungeni Aprili 10, 2026.
Kwa mujibu wa ukaguzi huo, uhaba huo mkubwa wa wataalamu unasababisha mzigo mkubwa kwa madaktari waliopo, ambapo daktari mmoja analazimika kuhudumia maelfu ya watoto wenye matatizo ya mfumo wa fahamu.
CAG amesema hali hiyo inaathiri ubora wa huduma, kuchelewesha uchunguzi na, wakati mwingine, kusababisha wagonjwa kukosa matibabu sahihi kwa wakati.
Ripoti hiyo inaeleza changamoto hiyo haipo Dar es Salaam pekee, bali imeenea katika mikoa mbalimbali nchini.
Kwa mfano, mikoa ya Tabora, Dodoma, Mwanza na Rukwa, yenye jumla ya takribani watoto 20,000 wenye matatizo hayo, haina hata daktari mmoja bingwa wa ubongo kwa watoto.
Katika upatikanaji wa wataalamu wa kuchunguza matatizo ya mfumo wa fahamu, pia madaktari bingwa wa mionzi walipatikana 83 kati ya 728 wanaohitajika, mafundi wa teknolojia ya mionzi 448 kati ya 4,223 wanaohitajika, wanasayansi wa mionzi 43 kati ya 252 wanaohitajika, na madaktari bingwa wa mfumo wa fahamu kwa watoto ni watatu tu nchi nzima.
“Kutokana na hali hiyo, wazazi na walezi wanalazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma katika hospitali za rufaa za kanda au taifa, hali inayoongeza gharama na kuchelewesha huduma kwa watoto wanaohitaji matibabu ya haraka,” amesema CAG.
Mbali na uhaba wa wataalamu, ukaguzi huo pia umebaini changamoto kubwa katika upatikanaji wa vifaa tiba muhimu kwa ajili ya uchunguzi wa matatizo ya mfumo wa fahamu.
Vifaa kama mashine za CT-Scan na MRI vinapatikana zaidi katika hospitali za ngazi ya juu, huku hospitali za mikoa na wilaya zikiwa na upungufu mkubwa wa vifaa hivyo. Pia, vifaa kama vile vichunguzi vya vinasaba havikupatikana kwa urahisi katika ngazi zote za hospitali.
“Kutokana na upungufu huo, watoto wengi wanapatiwa matibabu bila kufanyiwa uchunguzi wa kina unaohitajika kubaini aina halisi ya tatizo. Katika baadhi ya maeneo, wagonjwa wa kifafa wamekuwa wakipewa dawa bila vipimo vya uhakika, hali inayoweza kusababisha matumizi yasiyo sahihi ya dawa,” amebainisha CAG.
Aidha, ripoti imebainisha kuwa huduma za afya ya mfumo wa fahamu zimejikita zaidi katika hospitali za rufaa na za taifa, huku ngazi za chini zikiwa hazina uwezo wa kutoa huduma hizo ipasavyo. Hali hii imechangia kuwepo kwa msongamano mkubwa wa wagonjwa katika hospitali chache zinazotoa huduma hizo.
Changamoto nyingine iliyobainishwa ni kukosekana kwa mfumo wa kitaifa uliounganishwa wa takwimu za wagonjwa wenye matatizo ya mfumo wa fahamu. Mfumo uliopo kwa sasa unatumia mifumo mbalimbali isiyounganishwa, jambo linalofanya kuwa vigumu kupata takwimu sahihi za kitaifa na kupanga huduma kwa ufanisi.
Kutokana na mapungufu hayo, wataalamu wa afya wanashauri Serikali kuongeza uwekezaji katika mafunzo ya wataalamu bingwa wa ubongo kwa watoto, pamoja na kuboresha miundombinu ya afya ili kuhakikisha huduma zinapatikana katika ngazi zote.
Pia wanasisitiza umuhimu wa kusambaza vifaa tiba katika hospitali za mikoa na wilaya, ili kurahisisha uchunguzi wa mapema na kupunguza mzigo kwa hospitali za rufaa.
Kwa upande wake, Serikali imekuwa ikiweka mikakati mbalimbali ya kuboresha sekta ya afya, ikiwemo kuongeza wataalamu na kuboresha huduma za kibingwa. Hata hivyo, ripoti ya CAG inaonesha bado kuna pengo kubwa linalohitaji kushughulikiwa kwa haraka ili kulinda afya na ustawi wa watoto nchini.
