Mahakama ya Rufani yaitoa Chadema kifungoni, rasmi kufanya siasa

Dar es Salaam. Mahakama ya Rufani imekiondolea kifungo cha kutofanya shughuli za kisiasa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) baada ya kuondoa zuio hilo lililowekwa na Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam.

Uamuzi huo wa kukiweka huru chama hicho na kukiruhusu kuendelea na shughuli zake za kisiasa umetolewa na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani, Jaji Augustine Mwarija, Jaji Issa Maige na Jaji Abraham Mwampashi, leo Jumatano, Aprili 15, 2026.

Uamuzi huo umetokana na mashauri ya mapitio ya Mahakama yaliyofunguliwa na Mahakama yenyewe kutokana na kesi ya msingi ya madai ya mgawanyo usio sawa wa rasilimali za chama hicho baina ya Bara na Zanzibar.

Kesi hiyo imefunguliwa Mahakama Kuu Dar es Salaam na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chadema, Said Issa Mohamed, pamoja na wajumbe wawili wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu.

Walalamikiwa ni Bodi ya Wadhamini waliosajiliwa wa Chadema na Katibu Mkuu wa chama hicho.

Walalamikaji wanadai kuwa kumekuwa na mgawanyo usio sawa wa mali za chama na rasilimali za kifedha kati ya Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara, kinyume na Sheria ya Vyama vya Siasa na Katiba ya chama hicho.

Wadai walifungua shauri dogo la maombi ya zuio la muda dhidi ya wadaiwa, wakitaka wasijihusishe na shughuli za kisiasa wala matumizi ya mali za chama mpaka kesi ya msingi itakapoamuliwa.

Mahakama, katika uamuzi wake uliotolewa Juni 10, 2025, ilikubaliana na maombi na hoja za wadai na kutoa amri hizo zilizoombwa, yaani iliamuru wadaiwa kutokujihusisha na shughuli za kisiasa na kutotumia mali za chama mpaka kesi ya msingi itakapoamuliwa.

Hata hivyo, Mahakama ya Rufani, baada ya kuitisha na kusikiliza mashauri ya mapitio ya mwenendo na uamuzi mdogo wa Mahakama Kuu kuhusiana na kesi ya msingi na mashauri madogo yaliyotokana na kesi hiyo, likiwemo la zuio hilo la kufanya siasa, imetengua uamuzi huo wa zuio.

Kwa mujibu wa mmoja wa mawakili wa Chadema, Dickson Matata, katika uamuzi huo Mahakama ya Rufani imesema kuwa Mahakama Kuu haikuwa sahihi kuendelea kutoa uamuzi wa maombi ya zuio wala kuendelea na usikilizwaji wa maombi hayo baada ya wakili wa Chadema kujiondoa katika kesi hiyo.

“Jambo hilo liliwanyima haki ya kusikilizwa kwa usawa wadaiwa (Bodi ya Wadhamini wa Chadema na Katibu Mkuu), ambao hawakuwepo mahakamani. Kwa mantiki hiyo, zuio hilo ni batili na linatenguliwa,” amesema wakili Matata akinukuu uamuzi huo wa Mahakama ya Rufani.