Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Aprili 15,2025, Sh166 bilioni zimelipwa kwa makandarasi wazawa.
Kauli hiyo ya Ulega, inajibu hoja za wabunge mbalimbali waliolalamikia kuwepo kwa makandarasi wanaodai kutolipwa fedha zao, hali inayowafanya baadhi yao kushindwa kuendelea na kazi.
Wabunge walitoa malalamiko hayo wakati wakichangia hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya mwaka 2026/27 ya Sh12.5 trilioni kuanzia Aprili 1, 2026 hadi inahitimishwa leo Jumatano, Aprili 15, 2026.
Katika michango yao, wabunge karibu wote waliopata nafasi ya kuchangia waliitaka Serikali kuweka msukumo wa kutosha kupatikana kwa fedha lakini kumalizia na kuendelea miradi mbalimbali ya barabara ambayo inakuwa kero hususan nyakati za mvua.
Katika mchango wake, Waziri Ulega amefafanua na kueleza kinachofanywa na Serikali kuhakikisha barabara zinajengwa, huku akisisitiza michango yote ya wabunge wameichukua na wanakwenda kuifanyia kazi.
“Kuanzia Januari hadi leo Aprili 15, jumla ya Sh166 bilioni zimelipwa kwa makandarasi wazawa ili kuwawezesha kuendelea na kazi na kuhakikisha fedha hiyo inazungumza nchini,” amesema.
Amesema Rais Samia Suluhu Hassan, amesisitiza wakati wanalipwa makandarasi kipaumbele kitolewe kwa wale wa ndani ili kuhakikisha fedha hizo zinaingia katika mzunguko nchini.
Sambamba na hilo, amezungumzia wasiwasi wa miundombinu ya Afcon, amesema utekelezaji wa miradi unaendelea na Sh17 bilioni zimetolewa kwa ajili ya kumlipa mkandarasi CCECC kuanza ujenzi.
“Tumepanga kuhakikisha miji yetu ya Dar es Salaam na Arusha, kwenye jambo hili la Afcon, ukiachilia mbali ujenzi tu wa miundombinu, itapendeza sana, tumetenga Sh40 bilioni zitakazosambaza taa kila kona,” amesema.
Pia, amesema Serikali itaendeleza kazi iliyoanzwa na miradi yote viporo haitaachwa, iliyosainiwa itapata malipo ya awali na yote itatekelezwa.
“Tumechukua michango yote tunakwenda kuifanyia kazi na tutakwenda kuijibu pia wakati wa hotuba ya Wizara ya Ujenzi,” amesema.
Kwa upande wa Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amesema wamepokea Sh40 bilioni kwa ajili ya kuwalipa makandarasi na kwa sasa waende kufanya kazi.
“Fedha zimekwishatolewa sisi tutasimamia, mkandarasi atakayezingua tutazinguana. Tunajua miradi inayoendelea 867 mijini na vijijini,” amesema.
Amesema hatolala usingizi kuhakikisha miradi yote iliyoanza inakamilishwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama.
Aweso amesema wamefanya tathmini na kubaini ili kutimiza malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, muhimu wawekeze kwa kuwawezesha watendaji, wasiwe watu wa visingizio.
Amesema wamejizatiti kuhakikisha wanatumia mifumo katika utoaji huduma, ili kukomesha upoteaji wa maji au kubambikia wateja bili za maji.
Amesema zaidi ya vijiji 10,000 vimeshafikiwa na huduma ya maji, vimebaki 1,575 na wameelekezwa ndani ya miaka mitano vikamilishwe na wananchi wapate huduma.
Kuhusu vyanzo vya maji, amesema wanakwenda kutumia Gridi ya Taifa ya Maji kuhakikisha wizara haibaki kuwa ya maji ya kunywa pekee.
