Global Publishers
April 16, 2026
0 Comments
Jeshi la Iran limetoa onyo kali likisema huenda likazuia shughuli za biashara katika Bahari ya Shamu (Red Sea), Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman iwapo Marekani itaendelea na kile inachokiita mzingiro wa kijeshi wa majini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyorushwa kupitia televisheni ya serikali ya Iran, mkuu wa kituo cha uongozi wa kijeshi nchini humo, Ali Abdollahi, amesema hatua yoyote ya Marekani kuendelea kuzuia au kuhatarisha meli za biashara za Iran itachukuliwa kama kitendo cha kuchochea uvunjaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano.
Amesema kuwa vikosi vya jeshi vya Iran havitaruhusu kabisa shughuli za uagizaji na usafirishaji wa bidhaa kuendelea katika maeneo ya Ghuba ya Uajemi, Bahari ya Oman na Bahari ya Shamu endapo hali ya mzingiro itaendelea.
Onyo hilo linakuja wakati mvutano kati ya Iran na Marekani ukiendelea kuongezeka, huku maeneo ya baharini ya kimkakati yakihusishwa zaidi na biashara ya mafuta na usafirishaji wa kimataifa.
Wachambuzi wa masuala ya usalama wanasema hatua kama hiyo ikitekelezwa inaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa usafirishaji wa kimataifa wa nishati na bidhaa kupitia njia hizo muhimu za baharini.