Dk Kigwangalla: Niliandika barua kujiuzulu ubunge

Dar es Salaam. Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla amesema misimamo na harakati zake za kusimama kwenye haki, viliwahi kumfikisha kwenye uamuzi wa kuandika barua ya kujiuzulu ubunge mwaka 2012.

Uamuzi wake huo, amesema ulitokana na kushambuliwa na wabunge wenzake wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika kikao chao cha chama (Party Caucas) wakimshutumu kufadhili madaktari kugomea kikao na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda wakati huo.

Katika simulizi hiyo, Dk Kigwangalla amesema anachukulia mashambulizi na shutuma hizo, vilitokana na historia yake ya kusimama upande wa haki wa kupambania masilahi ya madaktari, alipokuwa Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Kanda ya Dar es Salaam, kabla ya ubunge.

Dk Kigwangalla ambaye historia ya uongozi wake, ilianzia shuleni akiwa kiranja mkuu, chuoni akiwa Rais wa Serikali ya wanafunzi na kwenye taaluma akiwa Rais wa MAT Dar es Salaam, amesema kusimamia haki aghalabu kuna madhila.

Dk Kigwangalla, amesimulia hayo wakati wa mahojiano maalumu na Mwananchi, yaliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam.

Mwanasiasa huyo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), aliwahi kuwa mbunge wa Nzega Vijini kwa miaka 15 na ubunge wake ulikoma mwaka 2025.

Alipowania tena nafasi hiyo, alishindwa katika kura za maoni akipata 1,715 dhidi ya Neto Kapalata aliyepata kura 2,570 na kuteuliwa na chama hicho kugombea Nzega Vijijini.

Pia, aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto na baadaye Waziri wa Maliasili na Utalii, hadi Juni 2020, akiwa amehudumu kwa miaka mitatu tangu Oktoba mwaka 2017 alipoteuliwa na Rais wa wakati huo, hayati John Magufuli.

Katika mahojiano hayo, mwanazuoni huyo mwenye shahada ya uzamivu ya afya ya jamii, amesema ndani ya kipindi cha uongozi wake wa MAT kuna mwaka ilifanyika migomo zaidi ya 10 ya madaktari, wakishinikiza kuthaminiwa na kupewa haki.

Kwa kuwa yeye ndiye aliyekuwa kiongozi wa Kanda ya Dar es Salaam iliyokuwa na zaidi ya asilimia 80 ya wanachama wote nchini, amesema hakukuwa na namna ya kumtenganisha na migomo iliyokuwa inafanyika, kwa maana aliiongoza.

Lakini, amesema migomo hiyo ilifanyika kudai haki za wanataaluma hao zilizokuwa zinaminywa, wakati huo yeye akiwa daktari mchanga baada ya kutoka chuoni na hata hakuwa ameajiriwa moja kwa moja.

Ameeleza baadaye aliachana na uongozi wa MAT na mwaka 2010 akaenda kuwania ubunge wa Nzega Vijijini kupitia CCM, akashinda na kuingia katika jukwaa la uongozi wa siasa za kitaifa.

Akiwa mpya kwenye siasa na ubunge, amesema alipata nafasi ya kuwa mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Huduma za Jamii, ambayo ndani yake kuna sekta ya afya.

Dk Kigwangalla, amesema wakati huo migomo ya madaktari haikuwa imeisha, ulifanyika mwingine ambao kamati ambayo yeye alikuwa mjumbe wake, ilipewa jukumu la kwenda kuwasikiliza madaktari ambao hata hivyo hawakutaka.

Kilichofanyika, amesema kwa kuwa kamati hiyo ilikuwa na wabunge ambao ni madaktari akiwemo yeye, waliamua kwenda kwenye kikao cha madaktari kama wanachama wa MAT ili wasikilize hoja na kupeleka mrejesho kwa kamati.

Katika kikao hicho, amesema alihudhuria aliyekuwa Naibu Waziri wa Afya wakati huo, Dk Lucy Nkya.

“Tulipata nafasi ya kuingia na kusikiliza hoja zote. Alikuwepo pia Naibu Waziri wa Afya, Dk Lucy (Nkya), wakati anatoa majibu yake madaktari hawakuridhishwa, hasira zikazidi wakamfukuza tunashuhudia yote, tukaenda tukatoa mrejesho,” amesema na kutoa ushauri kama kamati.

 Amesema kwa kawaida, wiki moja kabla ya kuanza Bunge, huwa wanakaa wabunge wa CCM kujadili yatakayokuja kwenye wiki hizo mbili za mkutano husika.

Kabla ya kikao hicho, amesema wakaambiwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda atakwenda kuzungumza na madaktari kuwasilikiza jijini Dar es Salaam, lakini alipokwenda ukumbini hakutokea hata daktari mmoja.

“Kuna baadhi ya madaktari ni rafiki zangu, nikawa nawauliza kwa nini mmefanya hivi si mngeenda kumsikiliza waziri mkuu anakuja na ofa gani, au ana jambo gani?” amesema.

Amesema majibu aliyoyapata ni kwamba kikao cha madaktari kiliamua kisiongee na kiongozi yeyote wa Serikali zaidi ya Rais mwenyewe wakati huo, Jakaya Kikwete.

Baada ya hilo kutokea, amesema ikabidi waende kwenye kikao cha Party Caucas ya wabunge wa CCM, ambacho waziri mkuu ndiye aliyekuwa kama mwenyekiti.

“Tuko kwenye kikao sasa… zilitokea lawama kubwa sana juu yangu…kwamba mimi ndio nimewagomesha madaktari wasiende kumsikiliza waziri mkuu.

“Baadhi ya wabunge wenzangu walinishambulia. Iliandikwa kwenye vyombo vya habari Kigwangalla atiwa kwenye kibano na ndio maana naisema kwa sababu ilishatoka hadharani,” amesema.

Amesema alishutumiwa na kutupiwa kila aina ya maneno bila kupewa nafasi ya kujitetea, ingawa baadhi walimtetea huku wajumbe wenzake wa kamati wakiishia kushangaa.

Mashambulizi, amesema yalikwenda mbali zaidi hadi ulifika wakati wengine wakapendekeza apelekwe kwenye kamati ya maadili ya CCM.

 “Sasa kilichosababisha yote hayo ni historia yangu ya nyuma kuwa kiongozi wa migomo na kusimama kwenye haki. Kile kitendo kiliniuma sana mpaka nikafikia hatua ya kuamua kuandika barua ya kujiuzulu ubunge na vyeo vyote nilivyokuwa navyo ndani ya chama,” amesema.

Hata hivyo, uamuzi wake wa kujiuzulu ulishindikana baada ya kukutana na wazee akiwemo Spika wa Bunge wa wakati huo, hayati Samuel Sitta na wengine waliomshauri ayazoee mambo hayo kwani ndivyo siasa ilivyo.

Amesisitiza yeye ni mtu anayependa kusimama kwenye haki na ukweli, kwa sababu anaamini haki mwisho wa siku itashinda.

“Mara zote mimi huwa nasimama kwenye haki ilimradi niwe kwenye misingi na niwe kwenye utaratibu. Kwa hivyo ndiyo maana mtu mwingine anaweza akachukulia kama vile ni misimamo mikali. Hapana,” amesema.

Dk Kigwangalla amesema hatua yake ya kuingia kwenye siasa anaamini ni kama asili yake, kwa kuwa maisha yake yote amekulia kwenye mazingira ya kiuongozi.

Akiwa mdogo, amesema alikuwa sehemu ya viongozi wa Chipukizi baadaye Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) na hata alipoingia shuleni, alikuwa kiongozi na chuoni alikuwa Rais wa Serikali ya Wanafunzi.

“Mara nyingi hata tukiwa na wenzangu wakisema nani hapa atakuwa kiongozi wa kundi hili, watanichagua mimi. Nimekuwa mtu wa kujenga mahusiano mazuri na wenzangu, marafiki na mwisho wa siku ikitokea fursa anatakiwa atumwe mtu kazi nimekuwa nikitumwa mimi,” amesema.

Uongozi kwake, amesema ulikuwepo hata alipoanza ajira, akachaguliwa kuwa Rais wa MAT Kanda ya Dar es Salaam, iliyokuwa na wanachama wengi zaidi.

Akiwa kiongozi MAT, amesema mwaka 2004 hadi 2005 kulipofanyika migomo zaidi ya 10, anaamini utulivu unaoonekana leo kwa wanataaluma ya udaktari, ulitokana na juhudi zao wakati huo.

“Sisi tulipambana kipindi chetu. Serikali ilirekebisha mambo mengi sana mpaka leo hii ukiwaona madaktari wametulia ujue jasho lilitutoka. Nilikuwa kitovu cha harakati zote hizo kipindi hicho kwa sababu mimi nilikuwa mwenyekiti wa chama,” amesema.