Mrithi wa Kapombe Simba huyu hapa!

BAADA ya beki wa kulia wa Simba, Shomari Kapombe kuitumikia timu hiyo kwa kipindi cha miaka tisa, mabosi wa kikosi hicho wameanza mchakato wa kutafuta mrithi wake, ambapo kwa sasa imetua kwa nyota wa Singida Black Stars, Ande Koffi Cirille.

Kapombe aliyejiunga na Simba Julai 1, 2017 akitokea Azam FC, amekuwa muhimili mkubwa wa kikosi hicho, ambapo kwa sasa mabosi wa timu hiyo wanataka kumtafutia mbadala wake, baada ya kudaiwa kutoridhishwa na kiwango cha David Kameta ‘Duchu’.

Beki huyo aliyetwaa mataji mbalimbali ikiwemo ya Ligi Kuu Bara mara nne mfululizo akiwa na Simba kuanzia msimu wa 2017-2018, 2018-2019, 2019-2020 na 2020-2021, amekuwa na mwenendo mzuri, ingawa anatafutiwa mtu atakayeleta changamoto mpya.

Sasa wakati mchakato huo ukiendelea, taarifa kutoka ndani ya timu hiyo zimeliambia Mwanaspoti miongoni mwa mabeki ambao wanaangaliwa ni wa Singida Black Stars raia wa Ivory Coast, Ande Koffi Cirille, anayemaliza mkataba mwishoni mwa msimu.

Cirille, aliyejiunga na Singida Julai 1, 2024, akitokea ASEC Mimosas ya kwao Ivory Coast, mkataba wake na kikosi hicho wa miaka miwili aliousaini unafikia tamati mwishoni mwa msimu huu, jambo linaloifanya Simba kuanza harakati za kumpata.

Chanzo kutoka ndani ya Singida, kimeliambia Mwanaspoti kwamba, nyota huyo aliyewahi kucheza FC LYS Sassandra ya kwao Ivory Coast, amewekewa mkataba mpya ili kuendelea kubakia, ingawa ameomba kufanya uamuzi huo utakapofika mwisho wa msimu.

“Mchakato wa kuboresha mkataba wake umefanyika lakini ameomba msimu uishe kwanza, hata sisi tumepata taarifa kutoka kwa mtu wake wa karibu akielezea dili la Simba, nadhani ndio maana amekuwa akisuasua kwenye hilo,” kilisema chanzo hicho.

Mwanaspoti linatambua uongozi wa Simba unafanya mazungumzo ya kimya kimya na wakala wa mchezaji huyo, Zambro Toure, kwa ajili ya kuipata saini yake, kwani ndiye pia aliyefanikisha usajili wa aliyekuwa nyota wa timu hiyo, Jean Charles Ahoua.

Uongozi wa Simba unaamini Cirille, aliyezaliwa Desemba 25, 1998, akiwa na miaka 27 kwa sasa, ni mtu sahihi kwa ajili ya kuleta changamoto mpya, huku suala la maslahi binafsi sio kikwazo, kwa sababu nyota huyo atakuwa huru mwisho wa msimu.

Mwanaspoti linatambua mabosi wa Simba wameanza mchakato wa kuboresha baadhi ya maeneo ya kikosi chao kwa msimu ujao, ambapo mbali na mbadala wa Kapombe, tayari inaelezwa imefikia makubaliano ya kumsajili kiungo mkabaji wa Pamba Jiji, Kelvin Nashon.

Katika msimu wake wa kwanza wa 2024-2025 akiwa na Singida, Cirille aliasisti mabao matatu ya Ligi Kuu huku, msimu huu wa 2025-2026, hadi sasa akiasisti mabao mawili, akisifika kwa uwezo mkubwa wa kuzuia na kutengeneza mashambulizi.