Mwanasiasa wa upinzani nchini Afrika Kusini, Julius Malema amehukumiwa kifungo cha miaka mitano jela baada ya kupatikana na hatia ya kumiliki kinyume cha sheria silaha ya moto na kufyatua hadharani.
Kwa mujibu wa BBC, mara baada ya hukumu hiyo kutolewa, wakili wa Malema aliwasilisha rufaa kupinga uamuzi huo, hatua iliyositisha kwa muda kupelekwa gerezani kwa kiongozi huyo wa chama cha Economic Freedom Fighters (EFF).
Urefu wa kifungo hicho unaweza pia kumfanya Malema, mwenye umri wa miaka 45, kupoteza sifa ya kuendelea kuwa mbunge.
Akiwa amesimama ndani ya Mahakama ya East London akiwa amevaa suti nyeusi na tai nyekundu, Malema hakuonyesha hisia zozote wakati Hakimu Twanet Olivier alipokuwa akisoma hukumu hiyo.
Mwaka jana, alitiwa hatiani kwa makosa matano, yakiwemo umiliki haramu wa silaha na risasi, kufyatua risasi katika eneo la umma pamoja na kuhatarisha maisha ya watu kwa uzembe.
Mashtaka hayo yanahusiana na tukio la mwaka 2018, ambapo video ilisambaa ikimuonyesha Malema akitumia bunduki kufyatua risasi kadhaa angani wakati wa maadhimisho ya miaka mitano ya chama chake yaliyofanyika katika mkoa wa Eastern Cape.
Katika utetezi wake, Malema aliiambia Mahakama kuwa silaha hiyo haikuwa yake, na kwamba alifyatua risasi hizo ili kuhamasisha umati wa watu, kwa mujibu wa tovuti ya habari ya SowetanLIVE.
Hata hivyo, katika uamuzi wake wa hukumu, Hakimu Olivier alisema kitendo hicho “hakikuwa cha ghafla… bali kilikuwa sehemu ya tukio la usiku huo,” kwa mujibu wa shirika la habari la Agence France-Presse.
Malema anafahamika kwa muda mrefu kama mwanasiasa mwenye misimamo mikali, mwenye mvuto mkubwa kwa wafuasi wake na anayesema wazi bila kificho.
