Arusha. Jeshi la Polisi mkoani Arusha linawashikilia watu sita kwa tuhuma za mauaji ya Askari Polisi, Roland Mollel, mkazi wa jijini Arusha.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Jeshi la Polisi mMoa wa Arusha leo Alhamisi Aprili 16,2026, Justine Masejo, imedai kuwa mauaji hayo yametokea jana Aprili 15,2026 usiku katika Mtaa wa Mlimani, Kata ya Muriet.
Kamanda Masejo amesema uchunguzi wa awali wa tukio hilo umebaini kuwa Roland akiwa anaendelea na shughuli zake binafsi baada ya kazi, kulitokea taharuki iliyotokana na kusambaa kwa maneno ya kundi la watu wakidai katika eneo lao kuna wezi wameonekana.
Amesema wakati hayo yakiendelea Roland akiwa anapita na mtu mwingine ambaye anadaiwa kuwa ni dereva bodaboda, aliyekuwa amempakiza kwenye pikipiki, kundi hilo lilianza kuwashambulia huku wakiwakimbiza.
“Msako bado unaendelea kluwatafuta watuhumiwa wengine ambao wamehusika na pia kukamilisha uchunguzi wa tukio hilo,” amesema Kamanda Masejo.
“Jeshi la Polisi linaendele kutoa wito kwa baadhi ya wananchi wanaoendekeza tabia za kuchukua sheria mkononi kwa kuongozwa na mihemko kwani kwa kufanya hivyo ni kuvunja sheria pamoja na kusababisha madhara kwa watu ambao hawana hatia,” amesema.