Dar es Salaam. Sekta ya bima nchini inatarajiwa kunufaika na ongezeko la ushindani, ubunifu na uaminifu wa watumiaji kufuatia uzinduzi wa mpango mpya wa tuzo za kitaifa unaolenga kuweka viwango vya juu vya utendaji sekta hiyo na kupanua fursa kwa wadau.
Mpango huo ujulikanao kama Tuzo za ATI Bima, umezinduliwa na Chama cha Wamiliki wa Kampuni za Bima Tanzania (ATI), ukizileta pamoja kampuni za bima, madalali, mawakala na watoa huduma za bima katika juhudi za kuinua ubora wa huduma.
Hii ni mara ya kwanza kwa tuzo hizo kutolewa nchini zikitajwa kuchochea ukuaji wa sekta hiyo ambayo licha ya umuhimu wake bado haijachangamkiwa kikamilifu.
Hatua hiyo inakuja wakati sekta ya bima ikiendelea kukua na kubadilika, ikichochewa na maboresho ya kanuni, upanuzi wa njia za usambazaji na matumizi ya teknolojia za kidijitali zinazorahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi wengi zaidi.
Akizungumza leo Aprili 16, 2026, Mwenyekiti wa ATI, Dk Flora Minja amesema tuzo hizo zinalenga zaidi ya kutambua mafanikio ya wadau wachache, bali kujenga utamaduni wa ubora unaogusa sekta nzima.
Amesema kupitia utambuzi wa utendaji bora na uongozi madhubuti, wadau watahamasika kubuni mbinu mpya zitakazochochea ukuaji wa sekta na kuongeza imani kwa watumiaji wa bima.
“Uwepo wa jukwaa la kitaifa la kutambua ubora utachochea uwazi, ushindani na utoaji bora wa huduma huku mchakato wa tuzo hizo ukitarajiwa kuendeshwa kwa mfumo huru wa tathmini ili kuhakikisha usawa na uaminifu,” amesema Dk Flora.
Tuzo hizo zitatolewa katika makundi mbalimbali ikiwemo Bima Bora ya Mwaka, Bima ya Maisha na Isiyo ya Maisha, pamoja na madalali, mawakala, kampuni za urejeshaji bima na watoa huduma.
Aidha, kutakuwa na tuzo binafsi kama Mtendaji Mkuu wa Bima wa Mwaka, Kiongozi Anayechipukia na Tuzo ya Mafanikio ya Maisha, huku makundi mengine yakitambua mchango wa teknolojia katika kuboresha huduma.
Kwa upande wake, Meneja wa Kanda ya Mashariki wa Mamlaka ya Udhibiti wa Bima Tanzania (Tira), Zakaria Muyengi amesema mpango huo pia una mwelekeo wa kijamii.
Ameeleza kuwa asilimia 10 ya mapato yatakayopatikana katika hafla hiyo yatatolewa kwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kusaidia matibabu ya watoto wenye matatizo ya moyo.
Ameongeza kuwa TIRA inaunga mkono mpango huo kwa kuwa utaongeza uelewa wa bima miongoni mwa wananchi na kuimarisha imani kwa watumiaji.
Katika miaka ya karibuni, sekta ya bima imeendelea kukua taratibu kutokana na mageuzi ya sera na juhudi za kuongeza matumizi ya bima kwa watu binafsi na biashara.
Mbali na utoaji wa tuzo, mpango huo pia utatoa nafasi ya majadiliano kwa wadau wa sekta hiyo kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano, kabla ya hafla ya kilele itakayowakutanisha watunga sera na viongozi kujadili mwelekeo wa wa sekta ya bima nchini.
