Wananchi wataka nembo ya BoT kwenye fomu za mikopo kudhibiti ‘mikopo umiza’

Mwanza. Wakati malalamiko ya wananchi kuumizwa na mikopo isiyo rasmi yakiongezeka, wakazi wa Wilaya ya Magu wamependekeza hatua mpya ya udhibiti, wakishauri fomu zote za mikopo ziwe na nembo ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ili kuwatambua wakopeshaji halali na kupunguza udanganyifu.

Wakizungumza leo, Aprili 16, 2026, katika mkutano wa utoaji elimu ya fedha kupitia programu ya “Zinduka Usiumizwe, Kopa kwa Maendeleo,” wananchi hao wamesema wengi wamejikuta kwenye madeni makubwa kutokana na kukopa bila uhakika wa uhalali wa taasisi zinazotoa huduma hizo.

Mkazi wa Mtaa wa National, John Lufega, amesema ukosefu wa utambulisho wa wazi kwa wakopeshaji umekuwa chanzo kikubwa cha wananchi kuingia katika mikataba hatarishi.

“Kwa mawakala wa benki unaona nembo zao wazi na unaamini, lakini kwa wakopeshaji wa mitaani hakuna utambulisho. Hapo ndipo wananchi wengi wanapodanganyika,” amesema Lufega.

Ameongeza kuwa kuwekwa kwa nembo ya BoT kwenye fomu za mikopo kutarahisisha utambuzi wa wakopeshaji wenye leseni na kujenga uaminifu kwa wateja.

Naye mkazi wa Magu mjini, Salome Paulo, amesema uzoefu unaonesha jinsi mikopo hiyo inavyoweza kumuingiza mtu kwenye matatizo makubwa ya kifedha kutokana na masharti magumu ya urejeshaji.

Baadhi ya wakazi wa Wilaya ya Magu wakipewa elimu ya mambo ya kuzingatia kabla ya kuchukua mkopo kuepuka mikopo umiza. Picha na Saada Amir

“Masharti ni magumu, ukichelewa kidogo tu unaongezewa faini kubwa. Wakati mwingine unajikuta unalipa zaidi ya mkopo wenyewe,” amesema Salome.

Ameeleza kuwa aliwahi kukopa na kurejesha kwa wakati, lakini baada ya kuugua alishindwa kuendelea na marejesho, na hivyo kuingia kwenye mzigo mkubwa wa faini.

Kwa upande wake, Meneja Usaidizi Uchumi na Takwimu wa BoT Kanda ya Mwanza, Paul Lawuo, amesema taasisi hiyo inaendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kuhakikisha wanakopa katika taasisi zilizosajiliwa na zenye leseni halali.

Amesisitiza kuwa kisheria hairuhusiwi mtu au taasisi kutoa mikopo bila kuwa na leseni kutoka BoT, na kwamba hatua kali za kisheria huchukuliwa dhidi ya wanaokiuka taratibu hizo.

“Kukopa kwenye taasisi zilizosajiliwa kunampa mwananchi ulinzi zaidi, kwa sababu anakuwa na mahali pa kukimbilia endapo kutatokea mgogoro,” amesema Lawuo.

Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Magu, Zubeir Daud, amesema ukosefu wa elimu ya fedha umechangia wananchi wengi kuingia kwenye mikopo isiyo rasmi inayowaumiza kiuchumi.

“Ofisi ya mkuu wa wilaya inapokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi waliokopa kwenye taasisi zisizo na leseni na baadaye kukumbana na masharti magumu,” amesema Daud.

Katibu Tawala Wilaya ya Magu, Zubeir Daud akizungumza wakati wa utoaji wa elimu kwa wananchi wilayani Magu kuhusu mambo ya kuzingatia kabla hawajakopa kupitia programu ya Zinduka Usiumizwe. Picha na Saada Amir

Amebainisha kuwa elimu inayoendelea kutolewa inalenga kuwasaidia wananchi kuelewa riba, gharama za mikopo na sehemu salama za kukopa ili kufanya maamuzi sahihi ya kifedha.

Kutokana na hali hiyo, wananchi wameaswa kuhakikisha wanachunguza uhalali wa mkopeshaji, kuelewa masharti yote ya mkopo na kuepuka mikopo inayotolewa kupitia njia zisizo rasmi, huku wakihimizwa kukopa kwa malengo ya maendeleo badala ya matumizi yasiyo na tija.