Watu 61 mbaroni kwa tuhuma ya kuvunja sheria

Mwanza. Jeshi la Polisi jijini Mwanza linawashikilia watu 61 kwa tuhuma za kujihusisha na matumizi na biashara ya dawa za kulevya, kukiuka masharti ya leseni za biashara, pamoja na kupatikana na dhana haramu za uvuvi katika Wilaya za Ilemela na Ukerewe.

Watu hao wamekamatwa katika   operesheni maalumu ya kuwatafuta wahalifu na wanaotumia dawa za kulevya (bangi).
Katika taarifa hiyo iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna wa Polisi, Wilbrod Mutafungwa, leo Aprili 16, 2026 kwa waandishi wa habari amesema wanashirikiana na wananchi kufanikisha operesheni hiyo.

“Watu 16 wamekamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya (bangi) pamoja na kupatikana na bangi hizo Wilaya ya Ukerewe. Watuhumiwa watatu wamekamatwa kwa tuhuma za kupatikana na zana haramu za uvuvi zikiwamo timba na kokoro la kuvulia chambo, huko kata ya Murutunguru, Wilaya ya Ukerewe.”

Aidha jeshi hilo limewakamata watu 15 kwa tuhuma za kukiuka masharti ya leseni za biashara katika baa na nyumba za kulala wageni katika Wilaya ya Ilemela, makosa hayo yanachochea vitendo vya kihalifu.

Pia usiku wa Aprili 15, katika  eneo la Kona ya Bwiru, Villa Park na Furahisha, Wilaya ya Ilemela waliwakamata wanawake 16 wanaojihusisha na kujipatia fedha kwa kuuza miili yao pamoja na wanaume 11 waliokuwa wateja kwa wanawake hao.

Amesema  watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani kukabiliana na mkono wa sheria.

Aidha miongoni mwa vielelezo vilivyokamatwa katika operesheni hizo ni pamoja na dawa za kulevya aina ya bangi zenye uzito wa kilogramu 13.5, makokoro matano, pamoja na vifaa mbalimbali vinavyotumika katika vitendo vya uhalifu.

Taarifa hiyo imeeleza operesheni hizi ni endelevu katika wilaya zote saba za Mkoa wa Mwanza, kwa lengo la kuhakikisha wahalifu wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.