Arusha. Wananchi wa Jiji la Arusha wameilalamikia tabia ya baadhi ya madereva wa daladala kukatisha safari, wakisema inaongeza gharama za usafiri na kuwaumiza kiuchumi, hasa katika kipindi ambacho nauli zimepanda bila mwongozo rasmi.
Wakizungumza na Mwananchi leo, Aprili 16, 2026, wakazi hao wameiomba Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) kuingilia kati hali hiyo na kuwalazimisha watoa huduma kwa kuzingatia masharti ya leseni zao, ikiwemo kuwafikisha abiria hadi mwisho wa safari.
Malalamiko hayo yanakuja wakati kukiwa na ongezeko la bei ya mafuta duniani na nchini, hali iliyosababisha baadhi ya watoa huduma kupandisha nauli bila idhini ya mamlaka husika, huku wakidaiwa pia kukatisha safari ili kuongeza mapato.
Wakazi wa eneo la Mapambazuko, Kata ya Terrat, wamesema mwenendo huo ni kinyume cha haki za abiria na umeongeza mzigo kwa wananchi wa kipato cha chini.
Mmoja wa wakazi hao, Jane Muya, amesema licha ya nauli rasmi kutoka Soko la Kilombero hadi Mapambazuko kuwa Sh800, kwa sasa imekuwa Sh1,000, huku madereva wakishindwa kufikisha abiria mwisho wa safari.
“Tupo tayari kulipa nauli iliyoongezeka, lakini kinachotusumbua ni kukatishiwa safari njiani na kulazimika kupanda bajaji kwa Sh700 ili kufika nyumbani,” amesema.
Kwa upande wake, mkazi wa Intel, Kata ya Muriet, John Melau, amesema pamoja na madereva kupanga nauli zao, bado hawatekelezi wajibu wa kuwafikisha abiria wanakotakiwa, jambo linalowaongezea gharama na usumbufu.
Ameongeza kuwa hali hiyo imekuwa changamoto kubwa kwa wanafunzi wanaochelewa kufika nyumbani, hivyo kuongeza hofu ya usalama kwa wazazi.
Wakazi wa jijini Arusha wakipanda daladala eneo la Soko la Kilombero linalofanya safari zake kati ya Nelson Mandela na Mapambazuko jana. Picha na Filbert Rweyemamu
“Serikali inapaswa kuangalia upya viwango vya nauli vinavyoendana na hali halisi ya maisha ya wananchi, lakini pia kudhibiti vitendo vya ukiukwaji wa masharti ya leseni,” amesema.
Naye Charles Mollel, mkazi wa Oljoro, amesema tabia ya kukatisha safari imekuwa ikijitokeza zaidi nyakati za jioni, na baadhi ya madereva huamua kuishia njiani ili kufanya mizunguko mingi zaidi.
Ametaja maeneo ya Kwamrombo kuwa miongoni mwa vituo ambavyo daladala zinazofanya safari kati ya Soko la Kilombero na Dambo zimekuwa zikikatisha safari, licha ya nauli inayotozwa kuweza kufikisha abiria hadi mwisho wa safari.
Juhudi za kumpata Meneja wa Latra Mkoa wa Arusha, Omary Salum, ili kuzungumzia suala hilo hazikufanikiwa, baada ya simu yake kuita bila kupokelewa, na ujumbe mfupi wa maandishi kutopatiwa majibu.