MABINGWA watetezi wa Kombe la Muungano kwa mchezo wa Nage, Fighters Nage Queens wamesema wako tayari kutetea ubingwa wao katika mashindano yatakayofanyika Aprili 23 hadi 27 mwaka huu.
Mashindano hayo yatakayofanyika jijini Dar es Salaam yanatarajiwa kushirikisha timu 20 na 17 zitatoka Dar es Salaam na tatu kutoka Zanzibar.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mratibu wa Mawasiliano wa timu hiyo, Ali Bakari ‘Cheupe’, amesema maandalizi ya kikosi hicho yako vizuri.
“Tupo tayari kuutetea ubingwa wetu. Timu inaendelea na mazoezi ili kuhakikisha tunakuwa katika kiwango bora,” amesema.
Ameongeza, wanaliamini benchi la ufundi na ushirikiano kutoka kwa wazazi pamoja na viongozi wa timu hiyo, kwani lengo la timu hiyo ni kulirejesha kombe hilo visiwani Zanzibar na kuipa heshima timu ya Fighters Nage Queens.
Amesema, sababu ya kushiriki kwenye mabonanza ya aina hiyo ni kuifanya timu hiyo itambulike zaidi na kupata nafasi kucheza nchi jirani.
