Madaktari bingwa bobezi wawasili nchini kutoa huduma, yumo wa tiba za asili

Dodoma. Hospitali ya Benjamin Mkapa imepokea madaktari bingwa bobezi watano kutoka China ili kuboresha utoaji wa huduma za kibingwa kwa Watanzania huku magonjwa lengwa yakitajwa ni Moyo ubongo, mifupa, mionzi na tiba asili.

Mpango huo wa miaka miwili pia utahamishia ujuzi kwa wataalamu wa ndani ili kuongeza idadi ya wanaonufaika na huduma hizo nchini ambapo mpaka kufikia sasa zaidi ya Watanzania 500 wamenufaika na huduma hizo zilizotolewa kwenye hospitali za Muhimbili na Mwananyamala jijini Dar es salaam.

Akizungumza wakati wa mapokezi ya madaktari hao hospitalini hapo leo Ijumaa, AprilI, 17, 2026 Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo, Profesa Abeli Makubi amesema lengo la ujio wa madaktari hao ni kuboresha utoaji wa huduma za udaktari bingwa nchini na katika hospitali hiyo ambayo imejikita kwa huduma za Kimatifa.

“Tutashirikiana na wataalamu hawa kutoka China, kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma bora kwa Watanzania wanaosumbuliwa na matatizo haya, na kupanua wigo wa matumuzi ya tiba mbadala katika kukabiliana na matatizo ya afya kwa wanchi wetu,” amesema Profesa Makubi.

Profesa Makubi ameeleza kuwa mpango huu pia utahusisha uhamishaji wa utaalamu wa utoaji huduma bobezi kutoka kwa wageni kwenda kwa wataalamu wa ndani waliopo katika hospitali hiyo ili kuongeza idadi ya madaktari wenye uwezo wa kutoa huduma hizo.

Mkurugenzi amesema uhamishaji wa utaalamu huo utafanyika kwa njia ya ufundishaji wa moja kwa moja utakaofanywa na wageni na ushirikiano baina ya wageni hao na wenyeji wakati utoaji wa huduma hizo ambapo wenyeji watajifunza kwa vitendo.

Kwa upande wake, mratibu wa huduma za tiba mbadala kutoka Wizara ya Afya, Marcello Kaijage amewakumbusha wataalamu hao kufanya kazi kwa kufuata miongozo ya serikali na taasisi husika ili kufanikisha azma ya ushirikiano huo.

Kaijage amewakumbusha madaktari wenyeji kuwa mabalozi wazuri kwa wageni na kuwapa ushirikiano wa kutosha utakaowasaidia kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na kuheshimu tamaduni za Kitanzania katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Niwakumbushe kufanya kazi kwa kufuata miongozo iliyowekwa na serikali, kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wageni ili kuimarisha utoaji wa huduma kwa Watanzania wenye tamamaduni tofautitofauti,” amesema Kaijage.

Naye, Kaimu Mganga Mfawidhi kutoka Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Dodoma, Dk Sarah Ludovick amesema ujio wa mtaalamu wa tiba za asili utaongeza chachu ya matumizi ya tiba hizo katika kukabiliana na magonjwa yanayowakumba Watanzania.