Asisti mbili za Okello zaibuka na jipya

MASHABIKI wa Yanga wanachekelea ushindi wa mabao 6-0 ilioupata timu yao dhidi ya Mbeya City kikiwa ni kipigo kikubwa cha pili msimu huu, kilichosababisha wapinzani wao hao kumfukuza kocha Mecky Maxime, lakini nyuma ya furaha hiyo kocha wa mabingwa hao watetezi ameibuka na staa mmoja wa kikosi chake akisema Allan Okello ni wa moto.

Kwenye mchezo huo licha ya mabao kufungwa na Pacome Zouzoua na Prince Dube waliofunga mawili kila mmoja, Maxi Nzengeli na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, lakini Okello alitengeneza asisti mbili ambazo zilimfanya Pedro kutamka maneno ya tahadhari kwa wapinzani wao juu ya kiungo huyo.

Asisti hizo alizowapa Maxi na Tshabalala kwenye mabao yao zimefanya Okello sasa kuwa staa aliyetengeneza pasi nyingi zaidi za mabao kwenye ligi akiwa nazo sita, akiwashusha wenzake Duke Abuya na Ellie Mpanzu waliokuwa wanaongoza kabla ya mchezo huo wa juzi kila mmoja akiwa nazo tano.

Akizungumza na Mwanaspoti, Pedro amesema Okello sasa yuko kwenye kiwango kizuri baada ya kuanza kuonyesha ufundi wake ambapo jicho la pasi zake limekuwa na hatari kwa wapinzani akijua kuwaangalia wenzake wakiwa maeneo sahihi.

Pedro amesema makali ya kiungo huyo hayapo tu kwenye mechi hizo bali amekuwa akifanya mambo kama hayo kwenye uwanja wa mazoezi akionyesha ubora mkubwa wa kujua wapi apeleke pasi zake ili wenzake wafunge.

“Unazungumza kuhusu Okello, nadhani sasa ameanza kuonyesha ule ubora ambao anao, huu sio uwezo wa muda mfupi ni daraja lake, unayoyaona anayafanya uwanjani kwenye mechi zetu anafanya hivyo hivyo kwenye uwanja wa mazoezi,” amesema Pedro.

“Sio mchezaji mbinafsi, anajua majukumu yake kama kiungo, angeweza kupiga golini lakini amekuwa akiangalia kwanza nani yupo kwenye eneo zuri afunge na hii ni alama ya mchezaji mwenye akili kubwa, tunao wengi hapa.”

Pedro aliongeza kuwa pasi ambazo Okello ameanza kuzipiga zitakuwa na faida kubwa kwa wachezaji wenzake hasa washambuliaji ambao kama wakitulia wataweza kufanya vizuri zaidi katika mechi za mashindano.

“Wachezaji wengi wanatengeneza sana nafasi, kabla ya mechi ya juzi tulikuwa na Duke aliyekuwa na asisti nyingi lakini muda huu tunazungumza kuhusu Okello, hii ina maana kwamba tunaweza kufunga mabao mengi zaidi kama washambuliaji wakiweza kutulia na kutumia nafasi.”

Dube ambaye alirejea kufunga akiandika bao lake la saba akizungumzia ubora wa Okello amesema kwa sasa mashabiki wataamini maneno yake aliposema Okello ni mchezaji wa daraja la juu ambapo bahati mbaya alichelewa kuanza kuonyesha makali yake.

“Kitu anachofanya Okello hapa watu wataamini kwamba nilisema huyu ni mchezaji wa daraja la juu, bahati mbaya ni kwamba alichelewa kuanza kufanya mambo ambayo tunayaona sasa, ni kiungo fundi sana,” amesema Dube.