Kocha Dodoma Jiji afuta mapumziko, kujipanga upya

BAADA ya Dodoma Jiji kupoteza mechi mbili mfululizo, kocha wa timu hiyo, Amani Josiah, amesema wachezaji wa kikosi hicho hawatakuwa na mapumziko, licha ya Ligi Kuu Bara kusimama ili kupisha Michuano ya Kombe la Muungano, inayoanza Aprili 21.

Michuano hiyo ya Kombe la Muungano inaanza rasmi kuanzia Aprili 21 hadi Aprili 29, visiwani Zanzibar, ambapo kwa upande wa Bara, inawakilishwa na mabingwa watetezi Yanga iliyochukua taji mwaka 2025, Simba, Azam FC na Singida Black Stars.

Kwa upande wa timu nne kutoka Zanzibar zitakazoshiriki michuano hiyo ni Mwembe Makumbi, Mafunzo FC, KVZ na Mlandege FC na kuhitimisha miamba minane watakaochuana katika mechi hizo zitakazopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex.

Akizungumza na Mwanaspoti baada ya mapumziko hayo, Josiah alisema kipindi hicho kitakuwa ni kizuri kwao ili kurekebisha changamoto mbalimbali zilizojitokeza, hivyo wachezaji wote wataendelea na programu za mazoezi isipokuwa wenye majeraha.

“Wiki moja huwezi kutoa mapumziko kwa wachezaji kwa sababu ni kipindi kifupi, tukumbuke baadhi ya wapinzani wetu ambao wanashiriki michuano hiyo wanaendelea kucheza, hivyo, ni lazima tuongeze ufanisi zaidi kikosini kwetu,” alisema Josiah.

Josiah aliyezifundisha Tunduru Korosho, Biashara United, Geita Gold na Tanzania Prisons alisema katika mechi mbili zilizopita walikosa balansi ya uzuiaji na ushambuliaji jambo analolifanyia kazi.

Katika mechi mbili zilizopita Dodoma ilianza kwa kuchapwa mabao 3-1 dhidi ya Simba katika hatua ya 16 bora ya Michuano ya Kombe la CRDB, Aprili 12, kisha kuchapwa tena kichapo kama hicho cha 3-1 katika Ligi Kuu na Coastal Union, Aprili 15.

Dodoma Jiji katika mechi 19, ilizocheza za Ligi Kuu kwa msimu huu wa 2025-2026, imeshinda sita, ikitoka pia sare sita na kupoteza saba, ikifunga mabao 18 na kuruhusu 21, ambapo timu hiyo ya ‘Walima Zabibu’ iko nafasi ya nane na pointi 24.

Katika hatua nyingine akizungumzia mechi iliyopita dhidi ya Coastal Union na mustakabali wa kikosi chao kuelekea mchezo ujao, kiungo wa timu hiyo, Mwana Kibuta alisema matokeo hayo yamewaumiza kwani hawakutarajia kutokana na matumaini na maandalizi waliyokuwa wameyafanya.

Alisema hesabu ilikuwa ni kushinda mchezo huo ili kuendelea kujivuta nafasi za juu, lakini kilichowakwamisha ni uchovu wa safari na nguvu kubwa iliyotumika katika mchezo dhidi ya Simba.

“Coastal Union wakajikuta wanatutawala mwanzo mwisho haswa kipindi cha kwanza, tulitumia nguvu nyingi mchezo dhidi ya Simba, lakini tukachoshwa pia na safari Arusha kuja Tanga.

“Matokeo haya yametuumiza sana japokuwa tumekubali kilichotokea na benchi la ufundi wametutuliza twende kujipanga upya kwa ajili ya mechi nyingine ili kuweza kufikia malengo yetu msimu huu,” alisema Kibuta.

Staa huyo raia wa DR Congo mwenye asisti mbili hadi sasa, ameongeza kuwa kinachowapa matumaini ni ari na morali kubwa iliyopo kikosini akibainisha kuwa mkakati wao ni kumaliza nafasi nne za juu.

Alisema baada ya kupoteza mchezo huo wanaenda kusahihisha makosa yao ili mechi inayofuata dhidi ya Namungo waweze kufanya kweli na kumaliza hasira zao kwakuwa watakuwa uwanja wa nyumbani.