Manyara. Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limetoa majiko 30 ya umeme kwa walimu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Manyara, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.
Majiko hayo yametolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Lazaro Twange yakilenga kuwapa motisha walimu katika kutekeleza majukumu yao na wakati huohuo, kuwahamasisha kutumia nishati safi ya umeme nyumbani na shuleni.
Akizungumza jana Aprili 18,2026 kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Fakii Lulandala amempongeza Twange kwa hatua hiyo, akisema inaunga mkono kwa vitendo ajenda ya Rais, Samia Suluhu Hassan ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Amesema mchango huo unaonyesha dhamira ya shirika katika kuboresha maisha ya wananchi kupitia matumizi ya nishati salama na rafiki kwa mazingira.
“Hatua hii itatoa motisha kwa walimu na kuongeza ufanisi wao kazini, kwani watatumia muda mchache kupika na hivyo kupata muda zaidi wa kufundisha wanafunzi,” amesema Lulandala.
Ameongeza kuwa mbali na mchango huo, Twange pia alishiriki kikamilifu katika kusimamia ujenzi wa shule hiyo alipokuwa Mkuu wa Wilaya ya Babati, jambo lililochangia kukamilika kwa miundombinu yake kwa wakati.
Kwa upande wake, Meneja wa Tanesco Mkoa wa Manyara, Mhandisi Regina Mvungi amesema majiko hayo yamekabidhiwa kwa walimu wote wa shule hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo.
Amesema walimu hao wanatarajiwa kuwa mabalozi wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa umeme katika jamii wanamoishi, wakiwemo wanafunzi na wananchi kwa ujumla.
“Lengo ni kuona matumizi ya nishati safi yanaenea zaidi, kuanzia shuleni hadi katika jamii inayotuzunguka,” amesema Mvungi.
Naye Mkuu wa Shule hiyo, Gisela Msoffe amelishukuru shirika hilo kwa msaada wake akisema majiko hayo yatasaidia kuokoa muda wa walimu na kuongeza ufanisi wao katika ufundishaji.
Amesema pamoja na zawadi hiyo, shule hiyo pia imenufaika na juhudi za kuhakikisha inapata huduma ya umeme katika majengo yake yote.
“Majiko haya yatatusaidia kuokoa muda wakati wa kupika na kutupatia nafasi zaidi ya kuzingatia majukumu ya kufundisha wanafunzi,” amesema Msoffe.
