BAADA ya kutambulishwa rasmi katika kikosi cha Napsa Stars ya Zambia, mshambuliaji wa Kitanzania Habib Kyombo ameanza kwa kasi kwa kufunga bao lake la kwanza akiwa na timu hiyo, jambo linaloonyesha huenda akaisaidia timu hiyo kusalia ligi kuu.
Napsa iko nafasi ya 16 kati ya timu 18 zinazoshiriki ligi ya Zambia na katika mechi 28, imeshinda sita, sare tisa na kupoteza 13 huku ikikusanya pointi 27.
Kyombo, ambaye alijiunga na klabu hiyo akitokea Mbeya City, mechi yake ya kwanza alicheza akitokea benchi dhidi ya FC Leopards na licha ya kutopata bao alionyesha kiwango kizuri kilichowavutia makocha wake.
Mechi ya pili dhidi ya Nkwazi FC, mshambuliaji huyo alipata nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza na kufunga goli ambalo liliisaidia Napsa kuondoka na pointi moja kutokana na sare ya bao 1-1.
Akizungumzia hilo, Kyombo amesema ana furaha kubwa kuanza kwa kufunga katika timu mpya na ameahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuisaidia timu kufikia malengo yake msimu huu.
“Ni mwanzo mzuri kwangu, nafurahi kufunga bao langu la kwanza, lakini kikubwa ni kuisaidia timu,” amesema Kyombo.
Aliongeza mazingira ya timu hiyo ni mazuri na wachezaji wenzake wamempokea vizuri, jambo ambalo limemsaidia kuonyesha uwezo wake uwanjani bila presha.
