Kocha Bai aachiwa msala African Sports

BAADA ya aliyekuwa Kocha wa African Sports ‘Wanakimanumanu’, Khalid Adam kuachana na timu hiyo, uongozi wa kikosi hicho umefikia makubaliano ya kumwajiri Kocha Ally Salimu Mdoe ‘Bai’, kuiongoza hadi mwisho wa msimu huu 2025-2026.

Akizungumza na Mwanaspoti, Bai amesema amefikia uamuzi wa kukiongoza kikosi hicho hadi mwisho wa msimu huu, huku lengo kubwa ni kuhakikisha pia anaipigania isishuke daraja, licha ya kazi kubwa aliyonayo kutokana na ushindani mkubwa uliopo.

“Nimeichukua timu katika kipindi kigumu sana ambacho ni cha kuipigania isishuke daraja, lengo ni kuhakikisha tunaepuka hilo, ila kama itashindikana kabisa, basi tumalize msimu tukishika nafasi za kucheza mechi za ‘Play-Off’,” amesema Bai.

Bai aliyeifundisha African Sports ikiwa Ligi Kuu Bara msimu wa 2015-2016 kabla ya kushuka daraja, anakuwa ni kocha wa tatu msimu huu kukifundisha kikosi hicho baada ya kuanza na Sharifu Joseph Ndokezi, kisha Khalid Adam aliyeondoka pia.

Kocha huyo anayemiliki Akademi ya Makorora ya Tanga, amewahi kuifundisha Tanesco (kwa sasa B19 FC), akikabiliwa na kibarua cha kuipambania Sports isishuke daraja, baada ya kikosi hicho kilichocheza mechi 22, kushika nafasi ya 14 na pointi 14.