Mbeya. Watu watano wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuhusika na mtandao wa wizi wa magari katika mikoa ya Mbeya na Songwe, baada ya kufanyika kwa operesheni maalumu kati ya Aprili 10 hadi 18, 2026.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana Jumamosi Aprili 18, 2026, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Athony Mkwama alisema watuhumiwa walikamatwa wakiwa na magari manne yanayodaiwa kuwa ya wizi.
Alisema operesheni hiyo ilifanywa kwa ushirikiano kati ya Polisi wa mikoa ya Mbeya na Songwe, ikiwa na lengo la kukabiliana na matukio ya uhalifu, hususan wizi wa magari.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Athony Mkwama akitoa taarifa ya kukamatwa kwa watuhumiwa watano wa wizi wa magari mikoa ya Mbeya na Songwe
Mkwama alidai kuwa mmoja wa watuhumiwa ni Lusekelo Kazimoto (25), maarufu Umeme Mwingi, mkazi wa Kasumulu wilayani Kyela, ambaye awali alisambaza taarifa za uongo mtandaoni akidai kuwa ametekwa.
Alidai Kazimoto alikamatwa akiwa na gari linalodaiwa kuwa la wizi aina ya Toyota Land Cruiser, ambalo lilikuwa limebadilishwa namba na injini.
Watuhumiwa wengine ni Gwakisa Kulyamo (31), mkazi wa Kilimahewa katika Mamlaka ya Mji wa Tunduma mkoani Songwe; Deus Mwamafupa (38), mkazi wa Kasumulu wilayani Kyela; Isack Luvanda (25), mkazi wa Tunduma; pamoja na Michael Ngonyani (36), mkazi wa Mtingimbole mkoani Ruvuma.
Ameyataja magari yaliyokamatwa ni pamoja na Toyota IST, Toyota Prado na Toyota Spacio. Alidai kuwa watuhumiwa waliyabadili magari hayo namba za usajili na injini kabla ya kuyasafirisha kwenda nchi jirani.
“Uchunguzi wa awali unaonesha watuhumiwa hawa ni sehemu ya genge linalojihusisha na wizi wa magari katika maeneo mbalimbali nchini,” alisema Mkwama.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi limeonya watu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu, hususan wizi wa magari, kuacha mara moja ili kuepuka hatua kali za kisheria.
Muonekano wa miongoni mwa magari ya wizi yaliyo kamatwa mkoani hapa
Wataka ulinzi shirikishi uimarishwe
Baadhi ya wananchi wameitaka Serikali kuimarisha mifumo ya ulinzi shirikishi ili kusaidia kupunguza matukio ya uhalifu.
Mkazi wa eneo la Nonde jijini Mbeya, Rehema Mwanjonde amesema kuna haja kwa Jeshi la Polisi kutoa elimu kwa viongozi wa Serikali za mitaa ili kuimarisha vikundi vya ulinzi wa jadi maarufu sungusungu.
Amesema mfumo huo uliwahi kuwa msaada mkubwa katika kudhibiti vitendo vya uhalifu, ikiwemo wizi na uvunjaji wa nyumba katika maeneo mbalimbali.
“Sungusungu miaka ya nyuma ilikuwa msaada mkubwa katika kukabiliana na matukio ya wizi wa kuvunja nyumba, ambayo sasa yanaanza kujitokeza tena katika baadhi ya maeneo,” amesema Mwanjonde.
