BAADA ya Mogbwemo Queens inayoshiriki Ligi ya Wanawake Sierra Leone kutwaa ubingwa wa ligi mapema, kiungo Mbongo, Zuwena Aziz ‘Zizou’ amesema ilikuwa lazima wanyakue taji kutokana na mwendelezo mzuri waliokuwa nao.
Mogbwemo Queens imebeba taji hilo ikiwa bado na mechi nne mkononi, hatua inayoonyesha ubora wao mkubwa msimu huu.
Ubingwa huo umeifanya timu hiyo kukata tiketi ya kutafuta nafasi ya kushiriki michuano ya WAFU A kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake.
Akizungumza baada ya mafanikio hayo, Zizou amesema msimu huu umekuwa wa kipekee kwake, akifurahishwa na kiwango alichoonyesha katika ligi hiyoyenye ushindani mkubwa.
“Narudi nyumbani ndani ya wiki hizi, mama yangu anaumwa, lakini msimu huu umekuwa bora sana kwangu, nimepata nafasi ya kucheza nikiwa kwenye ligi ngumu,” amesema Zizou na kuongeza;
“Tamanio langu ilikuwa kucheza ligi ya mabingwa Afrika na nashukuru tumefanikiwa, ingawa inaweza kuwa ngumu kwangu kucheza kwa sababu narudi nyumbani kumuuguza mama.”
Mogbwemo Queens ilibeba taji hilo mapema baada ya Ram Kamara inayoshika nafasi ya pili kukatwa pointi tano kwa kosa la kuchezesha wachezaji watano wa kigeni kinyume na kanuni za ligi hiyo.
Kupunguzwa kwa pointi hizo kuliwapa nafasi Mogbwemo Queens kujihakikishia ubingwa bila kusubiri matokeo ya mechi zilizobaki.
