Ramani za kiikolojia zafungua fursa kwa wachimbaji wadogo

Morogoro. Matumizi ya ramani za kiikolojia yameanza kuonekana kuwa suluhisho la kuongeza tija kwa wachimbaji wadogo wa madini ya ujenzi na viwanda mkoani Morogoro, huku yakitajwa kusaidia kupunguza uharibifu wa mazingira na kuondoa imani potofu zilizokithiri katika shughuli za uchimbaji.

Hatua hiyo inakuja wakati wachimbaji wengi wakiendelea kutumia nguvu kubwa na rasilimali nyingi kutafuta madini bila mafanikio ya kuridhisha, hali inayochangiwa na ukosefu wa taarifa sahihi za kiikolojia.

Mtaalamu wa miamba na madini kutoka Ofisi ya ofisa Madini Mkazi Mkoa wa Morogoro, Asiwe Ngala amesema wachimbaji wengi hawatumii ramani za kiikolojia, jambo linalosababisha uchimbaji wa kubahatisha na uharibifu mkubwa wa mazingira.

Akizungumza leo Jumapili Aprili 19, 2026 katika mafunzo kwa wachimbaji wadogo wa madini ya ujenzi na viwanda mjini Morogoro, Ngala amesema ramani hizo husaidia kubaini muundo wa miamba, mwelekeo wa madini, kina chake na ubora wake.

“Wengi wanachimba katika maeneo yasiyo na madini kwa kukosa taarifa sahihi. Matokeo yake wanatumia nguvu kubwa bila mafanikio na kuharibu mazingira,” amesema Ngala.

Ameongeza kuwa matumizi sahihi ya taarifa za kiikolojia yanaweza kulinda milima, vyanzo vya maji na mazingira kwa ujumla yanayoendelea  kuathiriwa na uchimbaji usiozingatia utaalamu.

Kwa upande wake, Ofisa Programu kutoka Shirika la Maendeleo ya Uchimbaji Mdogo wa Madini Tanzania, Reheme Mkuli amesema mafunzo hayo yanatekelezwa kupitia mradi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa kushirikiana na Tume ya Madini katika mikoa ya Morogoro, Singida, Tanga na Dodoma.

Mkuli amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea wachimbaji uelewa wa sheria za madini, ulipaji kodi sambamba na mbinu bora za uchimbaji unaowajibika.

Aidha, amesema matumizi ya vifaa rahisi kama GPS yatasaidia kubaini maeneo yenye madini kwa usahihi.

Ameongeza kuwa taasisi kama GST na ofisi za madini za mikoa, zinamiliki ramani sahihi zinazoonesha maeneo yenye madini, hivyo wachimbaji wanapaswa kuzitumia kabla ya kuanza shughuli zao ili kuepuka hasara.

Katika upande wa uzoefu wa wachimbaji, Mwazani Juma (50) amesema awali alijihusisha na uchimbaji wa madini ya vito lakini alikumbana na changamoto, ikiwemo imani potofu zilizowazuia wanawake kushiriki kikamilifu katika shughuli za uchimbaji.

Amesema baada ya kugunduliwa kwa mawe meupe yanayotumika katika ujenzi na viwanda, wachimbaji wengi wamehamia kwenye madini hayo kutokana na ushindani mdogo na fursa ya kipato.

“Zamani tuliamini mwanamke akiwa katika hedhi anaweza kufanya madini yapotee, lakini sasa tumeelewa kuwa si kweli,” amesema Mwazani.

Hata hivyo, wachimbaji bado wanakabiliwa na matatizo mbalimbali, ikiwemo ukosefu wa vifaa bora vya kazi. Lucy Abdallah (30) amesema hulazimika kutumia vifaa duni vinavyosababisha majeraha ya mikono na madhara ya vumbi.

Lucy amesema wengi wao hawana uwezo wa kumudu vifaa kinga kama glovu, miwani, barakoa na viatu maalumu, hali inayowaweka katika hatari ya kiafya.