Pina, shabiki wazichapa uwanjani | Mwanaspoti

TIMU ya Muembe Makumbi inayoshiriki Ligi Kuu Zanzibar, haiachi vituko kwenye ligi hiyo kuanzia mashabiki hadi wachezaji wake na mara nyingi imekuwa ikipokea adhabu kutoka Bodi ya Ligi Zanzibar kutokana na matukio ya utovu wa nidhamu.

Licha ya kupata adhabu hizo ikiwemo kufungiwa kwa mashabiki, lakini bado inaendeleza vituko vyake kwa kutoa kauli zisizofaa kwa wachezaji na waamuzi.

Aprili 18 mwaka huu, katika hali isiyo ya kawaida baada kumalizika kwa mechi ya Ligi Kuu Zanzibar ambayo Mlandege iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Muembe Makumbi kwenye Uwanja wa Mao A kisiwani Unguja, mshambuliaji wa Muembe Makumbi, Abdallah Iddi Mtumwa ‘Pina’ alitoka uwanjani na kumfuata shabiki wa Mlandege, maarufu kwa jina la Mbaba, kisha kuanza kupigana.

Haikufahamika chanzo cha ugomvi huo ambao mwisho wa siku watu waliingilia kati na kuwaachanisha.

Akizungumzia tukio hilo, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Zanzibar, Issa Kassim, amesema kwa mujibu wa kanuni nambari 20 (3) ya mashindano ya 2025-2026, mchezaji yeyote atakayefanya vitendo vya utovu wa nidhamu anatakiwa kufungiwa kuanzia michezo mitatu hadi mitano mfululizo.

“Kitendo alichofanya mchezaji huyo (Pina) ni utovu wa nidhamu na kufanya fujo kwasababu haitakiwi kwa kiongozi, mchezaji wala shabiki kufanya fujo kabla, wakati na baada ya mchezo,” amesema.

Ameongeza kuwa, kanuni hiyo imeeleza kuwa ikiwa mchezaji huyo atafanya uharibifu, anapaswa kulipia gharama zote.

Mshambuliaji huyo aliyekuwa akikipiga Mlandege msimu wa 2024-2025, alijiunga na Muembe Makumbi dirisha dogo la usajili msimu huu akitokea Pamba Jiji ya Ligi Kuu Bara.

Pina ambaye alisajiliwa na Pamba Jiji dirisha kubwa la usajili msimu huu 2025-2026 akitokea Mlandege ambapo aliibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Zanzibar 2024-2025 akifunga mabao 21, hakucheza mechi yoyote hadi anaondoka kikosini hapo na kurejea Ligi Kuu Zanzibar.