Dar es Salaam. Chama cha ACT Wazalendo kimeshauri Serikali na wadau mbalimbali kuchukua hatua tano muhimu kushughulikia ubadhirifu na upotevu wa fedha za umma ulioainishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ikiwemo kuwachukulia wahusika hatua kali za kisheria.
Chama hicho kimesisitiza watumishi wote wanaohusika na kuwezesha kuwepo na kushamiri kwa vitendo vya ubadhirifu na upotevu wa mapato wakamatwe.
Mapendekezo ya chama hicho yametolewa leo, Jumapili, Aprili 19, 2026, kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Ado Shaibu, katika mkutano na waandishi wa habari, wakitoa mapendekezo baada ya kufanya uchambuzi wa ripoti ya CAG.
Jambo la pili ambalo Ado amependekeza ni vyombo vya habari na asasi za kiraia kutekeleza wajibu wao wa kimapambano wa kuangazia, kumulika na kuweka hadharani vitendo vya ubadhirifu na upotevu wa fedha za umma.
“Tuna itaka Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa) ishughulikie makosa makubwa ya ufisadi na rushwa kwa uwazi. Serikali ihakikishe mifumo ya kielektroniki inafanya kazi kwa ufanisi na wakati wote,” amesema.
Pendekezo lingine lililotolewa na chama hicho ni kuwataka wananchi kutumia ripoti ya CAG kuwahoji, kuwakosoa na kuwazomea viongozi wabadhirifu, kupinga ufisadi na kulinda kila shilingi inayotokana na kodi zao.
Viongozi wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu (katikati), Makamu Mwenyekiti Bara, Issihaka Mchinjita (kushoto) na Katibu Mkuu Ado Shaibu (kulia) ambao wameshiriki kwenye uwasilishaji wa uchambuzi wa Ripoti ya CAG uliofanyika Makao Makuu ya ACT Magomeni Dar es salaam.
Machi 30, 2024, alipokuwa akipokea ripoti za CAG na Takukuru za mwaka 2025, Rais Samia Suluhu Hassan alisema Serikali itazifanyia kazi dosari zilizobainishwa na taasisi hizo ili zisijirudie mwaka ujao.
Akizungumzia eneo la kodi, Ado amesema CAG amebaini ongezeko la mashauri ya kodi kutoka kesi chache mwaka 2019/20 hadi zaidi ya mashauri 1,200 mwaka 2024/25 kwa Tanzania Bara pekee.
Amesema ongezeko hilo linaashiria udhaifu katika mifumo ya usimamizi wa kodi.
“Serikali inapaswa kurejesha imani ya walipakodi kwa kujenga mfumo wa kodi wa haki na unaotabirika. Mfumo wa kodi unapokuwa wa haki, migogoro inapungua na mapato yanaongezeka kwa uendelevu,” amesema.
Katika hilo, amewataka wafanyabiashara kuitumia ACT Wazalendo kuwasilisha kero zao ili kuweka msukumo wa kisiasa katika kudai mabadiliko dhidi ya ukandamizwaji wanaodai kufanyiwa.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Bara, Issihaka Mchinjita, amesema CAG amebaini miradi katika sekta za barabara, afya, maji na miundombinu kutelekezwa.
Hali hiyo imetokana na uzembe, ufisadi na ukosefu wa usimamizi, pamoja na viongozi wasiojali maisha na thamani ya fedha.
“ACT Wazalendo tunataka wahusika wote wa kusimamia miradi iliyokwama, kutelekezwa au kusuasua wakamatwe, wahojiwe na kufikishwa mahakamani, pamoja na kufutwa kwa mikataba mibovu.
“Tunaitaka Serikali iwajibike kwa kila senti iliyotumika kwenye miradi iliyokwama,” amesema.
Katika sekta ya gesi, Mchinjita ameisihi Serikali kuweka jitihada za makusudi katika miradi yote ya gesi asilia, ikiwemo utafiti, uzalishaji na usambazaji, na kwamba wote waliothibitika kufanya ubadhirifu au hujuma wachukuliwe hatua.
Naye Kiongozi wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu, amesema ili kuboresha utendaji wa Bohari ya Dawa (MSD) kutokana na dosari zilizoibuliwa na CAG, Serikali ilipe madeni yote inayodaiwa na bohari hiyo ili kuiwezesha kufanya kazi kwa ufanisi.
Kiongozi wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu wakati akizungumzia kuboresha utendaji wa Bohari ya Dawa (MSD) kutokana na dosari zilizoibuliwa na ripoti ya CAG
“Serikali ianze utaratibu wa malipo ya fedha taslimu na kwa wakati kwa ajili ya ununuzi wa dawa ili kuimarisha mtiririko wa fedha wa MSD.
“Pia, yafanyike mageuzi makubwa ya kimfumo na kiutendaji ndani ya MSD ili kudhibiti mianya ya ubadhirifu na uzembe,” amesema.
Mbali na hayo, Semu amesema hatua za kisheria zichukuliwe kwa watendaji wote walioshiriki katika uzembe, upotevu na manunuzi yasiyo na tija.
Pia, ameshauri kuteuliwa kwa watendaji wenye weledi, uadilifu na uzalendo ili kurejesha imani ya wananchi katika taasisi hiyo.
Kuhusu upotevu wa maji, Semu amesema Serikali itenge bajeti ya angalau Sh10 trilioni ndani ya miaka mitano (wastani wa Sh2 trilioni kila mwaka) kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya maji safi na majitaka nchini.
Pia, mamlaka za maji ziboreshe haraka miundombinu yake ili kudhibiti upotevu wa maji unaosababisha hasara kubwa kwa taifa.
Katika eneo la upotevu wa maji, mwishoni mwa Machi 2026, wakati wa uzinduzi wa ripoti ya utendaji wa mamlaka za maji safi na usafi wa mazingira kwa mwaka wa fedha 2024/25, Waziri wa Maji, Juma Aweso, alipendekeza mamlaka za maji kuanzisha vikosi kazi maalumu vitakavyosimamia udhibiti wa upotevu wa maji pamoja na kuimarisha ushirikishwaji wa wananchi.
