Dar es Salaam. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imebaini vifaa vya ujenzi vya Chuo cha Serikali za Mitaa vyenye thamani ya Sh396.89 milioni vilivyonunuliwa mwaka 2022 havijatumika hadi Desemba 2025.
Kwa mujibu wa CAG, hatua hiyo ni kinyume cha Kifungu cha 5(2)(a) na (b) cha Sheria ya Ununuzi wa Umma, 2023, kinachoelekeza ununuzi wote kufanyika kwa kuzingatia thamani ya fedha na kukuza uchumi, ufanisi na tija katika matumizi ya rasilimali za umma.
Katika ripoti hiyo ya mwaka wa ukaguzi wa Tamisemi ya mwaka wa fedha 2024/25, imebainishwa kuwa hoja hiyo iliwahi pia kuripotiwa katika ukaguzi wa CAG uliofanyika mwaka 2022/23.
“Kutotumika kwa muda mrefu kwa vifaa hivyo kunaonesha mapungufu katika mipango na kutokuwa na uwiano kati ya ununuzi na utekelezaji wa miradi, kwani vifaa vilinunuliwa kabla ya kuhakikisha upatikanaji wa fedha za utekelezaji.
“Hali hii imesababisha fedha za umma kushikiliwa kupitia vifaa visivyotumika na kuviweka katika hatari ya kuharibika, kupotea au kupitwa na wakati, kinyume na misingi ya thamani ya fedha na matumizi bora ya rasilimali za umma,” imeeleza sehemu ya ripoti hiyo.
Leo, Jumatano, Aprili 15, 2026, Mwananchi limemtafuta Kaimu Mkuu wa chuo hicho, Dk Mashallah Yusuph, ambaye amesema ni hoja za kawaida za CAG na wameshayafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na mkaguzi huyo.
“Tumeshayafanyia kazi na tumeshamjibu CAG,” amesema Dk Yusuph.
Katika kuhakikisha changamoto hiyo inashughulikiwa, CAG amependekeza menejimenti ya chuo hicho kuratibu katika upangaji na bajeti kwa kuhakikisha ununuzi wa vifaa vya ujenzi unafanyika baada ya uthibitisho wa kupatikana kwa fedha na ratiba ya utekelezaji kuidhinishwa.
Aidha, CAG amependekeza menejimenti ya chuo hicho kuandaa mpango wa matumizi wa muda maalumu kwa vifaa vilivyopo na kuujumuisha katika mpango kazi na bajeti ya taasisi ili kulinda fedha za umma na kuzingatia kanuni za thamani ya fedha.
