Global Publishers
April 15, 2026
0 Comments
Rais wa Marekani, Donald Trump amedai kuwa China imekubali kutosambaza silaha kwa Iran, kauli ambayo imezua mjadala mpya katika siasa za kimataifa huku Beijing ikiendelea kukanusha tuhuma hizo.
Katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii Jumatano, Trump alisema China inafurahia hatua yake ya kufungua tena mlango wa usafirishaji katika eneo la Strait of Hormuz, na akaongeza kuwa hatua hiyo imechangia makubaliano ya China kutowapatia Iran silaha.
Hata hivyo, kauli hiyo imekuja wakati ambapo Wizara ya Mambo ya Nje ya China imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kwamba nchi hiyo haihusiki na utoaji wa msaada wa kijeshi kwa Iran. Msemaji wa wizara hiyo amekanusha taarifa hizo, akizitaja kama zisizo na msingi.

Kwa upande mwingine, Marekani imekuwa ikidai kwa muda mrefu kwamba China imekuwa na mchango usio wa moja kwa moja katika kuimarisha uwezo wa kijeshi wa Iran, hususan katika sekta ya teknolojia ya makombora kupitia vifaa vinavyoweza kutumika kwa matumizi mawili (dual-use components).
Uhusiano kati ya China na Iran umeendelea kuwa chini ya uangalizi wa karibu wa mataifa ya Magharibi, kutokana na ushirikiano wao wa kiuchumi na kiusalama katika miaka ya hivi karibuni.
Wachambuzi wa masuala ya kimataifa wanasema kauli za Trump zinaweza kuongeza mvutano wa kidiplomasia kati ya Marekani na Beijing, hasa katika kipindi ambacho masuala ya usalama wa Mashariki ya Kati na njia za usafirishaji wa nishati kama Strait of Hormuz yanaendelea kuwa nyeti duniani.