Kariakoo katika mtego wa hatari-1

Dar es Salaam. Ukitembea kwenye mitaa ya Kariakoo kuanzia asubuhi hadi jioni, macho yako hayapumziki kuona  magari, pikipiki, mikokoteni, baiskeli, watu wakipishana kwa mabega, sauti za wauzaji zikigongana na utasikia kelele nyingi mbalimbali.

Juu, majengo ya ghorofa yanaendelea kupanda, chini biashara zinaendelea kama kawaida, hakuna anayesimama.

Kariakoo, eneo linalochukuliwa kama dhahabu ya Tanzania kwa thamani ya ardhi yake, limekuwa kivutio kikubwa cha uwekezaji. Kila mwenye mtaji anataka kupata sehemu. Lakini katika mbio hizo za maendeleo, taratibu za ujenzi na usalama zimeachwa nyuma, badala yake hatari imekuwa sehemu ya maisha ya kila siku.

Katika Jiji la Dar es Salaam, Kariakoo inaendelea kushuhudia ongezeko kubwa la majengo ya ghorofa yanayojengwa kukidhi mahitaji ya nafasi za kibiashara.

Hata hivyo, nyuma ya kasi hiyo ya maendeleo, kuna taswira nyingine isiyoonekana kirahisi ya matumizi ya majengo ambayo bado yapo kwenye hatua za ujenzi kabla ya kukamilika na kukaguliwa rasmi na mamlaka husika.

Chini ya majengo hayo, wafanyabiashara wamefungua maduka, wateja wanaingia na kutoka, huku juu mafundi wakiendelea na kazi. Nyaya za umeme zikiwa wazi, vifaa vya ujenzi vimepangwa pembezoni mwa sakafu za juu na njia za dharura hazionekani.

Katika eneo lenye msongamano mkubwa wa watu na shughuli zisizokoma, matumizi ya majengo yanayoendelea kujengwa yamegeuka kuwa tishio kwa ustawi wa jamii na hatari kwa wengine.

Moja ya jengo linaloendelea kufanyiwa ukarabati Kariakoo.

Ujenzi unaoendelea sambamba na biashara, unaacha mianya mikubwa ya hatari kuanzia kuanguka kwa mbao, nondo na milunda, achilia mbali mifumo duni ya umeme hadi kukosekana kwa maandalizi ya kukabiliana na majanga kama moto au jengo kuporomoka.

Licha ya hatari hizo, shughuli za kila siku zinaendelea chini ya majengo hayo kana kwamba hatari hiyo ni sehemu ya kawaida ya Kariakoo.

Katika mazingira haya, ujenzi unaonekana kuendeshwa bila usimamizi madhubuti. Uwajibikaji wa wahusika wakuu unaendelea kufifia, huku sheria zilizopo zikionekana kubaki kwenye vitabu badala ya kutumika kulinda maisha ya binadamu.

Sheria ya Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 imeweka masharti ya wazi juu ya wajibu wa waajiri na makandarasi kuhakikisha usalama wa wafanyakazi na wananchi wanaozunguka maeneo ya ujenzi. Hata hivyo, utekelezaji wake umekuwa dhaifu.

Matokeo ya hali hii hayaishii kwenye hatari za maisha pekee, kwani kuna ajali ndogo na kubwa zinazotokea, ambazo husababisha hasara za mali, kusitishwa kwa biashara na kuibua hofu miongoni mwa wafanyabiashara na wateja.

Hali hiyo inadhoofisha imani ya umma katika usalama wa majengo ya biashara na kuhatarisha hadhi ya Kariakoo kama kitovu salama cha biashara, ndani na nje ya nchi.

Ukosefu wa ukaguzi wa kitaalamu na vyeti vya matumizi (Completion Certificate), unamaanisha majengo yanaanza kutumika bila uhakika wa uimara wake wala maandalizi ya kukabiliana na majanga.

Ajali zilizotikisa Kariakoo

Uchunguzi  wa Mwananchi wa zaidi ya miezi mitatu kuanzia Desemba 2025 hadi Februari 2026 unaonesha tatizo la matumizi ya majengo yanayoendelea kujengwa limekithiri katika mitaa ya Mchikichi, Aggrey, Congo, Nyamwezi na Sikukuu.

Katika mitaa hiyo miongoni mwa mingine, majengo mengi ya ghorofa tayari yanatumika kibiashara yakiwa bado yanajengwa.

Moja ya jengo linaloendelea kufanyiwa ukarabati Kariakoo.

Katibu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo Februari 3, 2026, Peter Mbilinyi, anasema mara nyingi wafanyabiashara huanza kutumia majengo kwa sababu wamepanga fremu za majengo kwenye ramani na kuhakikishiana na mjenzi.

“Wafanyabiashara wanapanga fremu hizi na kuamua kulipa malipo kabla jengo halijakamilika kwa makubaliano kuwa litakamilika baada ya siku fulani, likifikia hatua fulani wapangaji wanaingia na kuendelea na shughuli zao bila kusubiri ukaguzi,” anasema Mbilinyi.

Anasema njia hiyo imetumika kwa sababu wamiliki huanza kuhesabu kodi za wapangaji wao pindi inapofika tarehe husika, hivyo uhakikisha wanakamilisha maeneo tarajiwa ya wapangaji na kuruhusu shughuli kuendelea.

“Kiuhalisia ni vigumu kuhoji kama jengo limekaguliwa au la kwa sababu si wote wanaelewa hayo mambo ya kisheria na taratibu zake, ndipo wanapojikuta wametumbukia kwenye janga la upangaji wa majengo ya aina hiyo,” anasema.

Mbilinyi anasema kwa mji wenye idadi kubwa ya watu kama Kariakoo, kuna haja ya kushirikiana na mamlaka kuhakikisha sheria na kanuni za ujenzi zinafuatwa kwa uaminifu.

“Kama hakuna kanuni na usimamizi thabiti, hatuwezi kupata mpangilio mzuri, ni lazima kila mtu aheshimu sheria, awe ni mfanyabiashara, mjenzi au mwenye jengo na mamlaka husika,” anasema Mbilinyi.

“Kama sheria zikiheshimiwa kwa adabu na kusimamiwa kwa usahihi, basi malalamiko yote yataepukika, na wafanyabiashara wote wataweza kufanya kazi zao kwa amani.”

Hata hivyo, matumizi hayo yamekuwa chanzo cha ajali mbalimbali ikiwamo moto unaosababishwa na mifumo ya umeme isiyokamilika pamoja na kuanguka kwa vifaa vya ujenzi.

Ajali za moto na matukio ya kuanguka kwa vifaa vya ujenzi ziliripotiwa na Mwananachi katika Mtaa wa Aggrey na Msimbazi mwaka 2025 pamoja na ajali ya moto katika jengo la zamani la DDC Kariakoo na nyingine kwenye makutano ya Mtaa wa Aggrey na Sikukuu.

Katika eneo lenye msongamano mkubwa kama Kariakoo, tukio moja dogo linaweza kugeuka kuwa janga kubwa ndani ya dakika chache kutokana na idadi ya watu wanaokusanyika kwa wakati mmoja.

Baadhi ya wafanyabiashara wanakiri kuona hatari zinazowazunguka, lakini wanasema hawana budi kuzikubali. Shinikizo la kupata eneo la biashara Kariakoo ni kubwa kiasi kwamba hulazimika kufanya kazi katika mazingira yasiyo salama ili wasipoteze wateja na mitaji yao.

Mfanyabiashara wa vifaa vya umeme katika Mtaa wa Sikukuu, Abdulazack Hassan anasema kufanya biashara katika jengo linaloendelea kujengwa ni hatari, lakini ni uamuzi unaolazimishwa na hali halisi ya biashara Kariakoo.

“Unajua kabisa jengo bado linafanyiwa kazi, nyaya zipo wazi na hakuna ukaguzi, lakini ukisubiri likamilike unapoteza wateja, hapa Kariakoo ukichelewa kidogo tu, eneo linachukuliwa,” anasema.

Kauli hiyo inaungwa mkono na mfanyabiashara wa nguo katika Mtaa wa Congo, Shayba Karim anayesema ushindani mkali na gharama kubwa za upangaji hulazimisha wafanyabiashara kuingia mapema kwenye majengo hayo.

Kwa Happyness Sanga wa Mtaa wa Nyamwezi, kila siku ni maombi.
“Kila siku unaomba Mungu isije ikatokea ajali, ujenzi unaendelea juu, vifaa vinapita karibu na wateja, lakini biashara haziwezi kusimama,” anasema.

Hofu hiyo iligeuka kuwa tukio halisi kwa Pius Ndunguru wa Mtaa wa Aggrey aliyedondokewa na mbao na milunda kutoka juu ya ghorofa Novemba 7, 2025 na kujeruhiwa mkono. Tukio hilo lilithibitishwa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Mkoa wa Ilala, Peter Mabusi, aliyeeleza kuwa mtu mmoja aliokolewa akiwa hai baadaya kunaswa chini ya milunda.

Mnyororo wa uwajibikaji wakatika

Katika mazingira haya ya hatari yanayoendelea Kariakoo, swali linalojitokeza si uwepo wa sheria, bali nani anapaswa kusimamia utekelezaji wake. Majengo kwa asili yake, haina sheria moja ya moja kwa moja, bali yanasimamiwa na taasisi kadhaa zinazogawana majukumu.

Taasisi hizo ni pamoja na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (Osha), mamlaka za Serikali za mitaa, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na idara za mipango miji.

Kila taasisi ina wajibu maalumu wa kuhakikisha majengo hayaanzi kutumika kabla ya kukamilika na kukaguliwa, lakini kwa vitendo, majukumu hayo yanaonekana kugawanyika bila uwajibikaji wa moja kwa moja.

Matokeo yake, majengo yanaendelea kutumika huku kila taasisi ikionekana kusubiri nyingine ichukue hatua. Katika msongamano wa Kariakoo, pengo hilo la uwajibikaji ndilo linalogeuka kuwa hatari kwa wananchi.

Kwa mujibu wa Sheria ya Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003, kifungu cha 54, 55 na 73 vinaweka wajibu kwa mwajiri au mkandarasi kuhakikisha usalama wa wafanyakazi na wananchi waliopo karibu na eneo la kazi. Sheria inamtaka mkandarasi kuzuia hatari zote zinazoweza kujitokeza kutokana na ujenzi unaoendelea.

Kifungu cha 55 kinaeleza wazi hatua za kuzuia ajali, ikiwamo kufunga vizuizi kuzuia wananchi kuingia maeneo hatarishi, pamoja na kutumia neti au vizuizi vingine kuzuia vifaa vya ujenzi kuanguka.

Kifungu cha 73 kinataka vifaa vya ujenzi vipangwe ndani ya eneo la ujenzi ili kuzuia madhara kwa wananchi.

Lakini ukitembea Kariakoo, mara nyingi hakuna vizuizi. Hakuna neti. Hakuna alama za onyo. Badala yake, wananchi wanapita chini ya ujenzi unaoendelea, wateja wanaingia madukani na mafundi wanafanya kazi juu yao.

Kwa upande wa moto, Sheria ya Zimamoto na Uokoaji ya mwaka 2007 kupitia vifungu vya 30 na 31, inatoa mamlaka kwa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji kukagua majengo yanayoendelea kujengwa. Ukaguzi huo unapaswa kuhakikisha uwepo wa vifaa vya kuzimia moto, njia za dharura zisizozibwa na mifumo salama ya umeme.

Hata hivyo, majengo mengi Kariakoo yanaanza kutumika bila maandalizi hayo, hali inayoongeza hatari ya moto katika eneo ambalo tayari lina msongamano mkubwa wa watu na mali.

Pia, Sheria ya Serikali za Mitaa ya mwaka 1982 kupitia vifungu vya 55(1)(f) na 56, inazipa Manispaa mamlaka ya kusimamisha ujenzi wowote unaohatarisha usalama wa wananchi. Lakini licha ya mamlaka hayo, majengo yanayoendelea kujengwa yanaendelea kutumika kana kwamba hakuna mwenye jukumu la kusimamisha.

Baadhi ya wasimamizi wa majengo wanakiri kuwepo kwa matumizi ya mapema, wakieleza shinikizo la gharama kuwa ndilo linalowasukuma kufanya hivyo.

Wanasema ujenzi wa ghorofa Kariakoo unahitaji mtaji mkubwa na mara nyingi unahusisha mikopo ya benki yenye riba inayosoma kila mwezi, hivyo wamiliki kulazimika kuanza kukusanya kodi mapema.

Msimamizi wa moja ya majengo ya ghorofa katika Mtaa wa Aggrey anasema kusubiri jengo likamilike kikamilifu kabla ya kuanza matumizi kunachukua muda mrefu, wakati mikopo, kodi ya ardhi na gharama nyingine zinaendelea.

“Ujenzi unaweza kuchukua zaidi ya mwaka, lakini gharama hazisimami. Wakati mwingine mmiliki anaona ni heri aanze kutumia sehemu ya jengo ili kupunguza mzigo wa kifedha,” anasema huku akiomba hifadhi ya jina lake.

Wengine wanategemea kauli ya mkandarasi kuwahakikishia kuwa baadhi ya maeneo ni salama kutumika, licha ya kukosekana kwa ukaguzi wa mwisho wa kitaalamu na vyeti halali vya matumizi.

Kwa upande wao, makandarasi wanaotekeleza miradi ya ujenzi Kariakoo wanakiri kuwepo kwa ukiukwaji wa sheria, wakieleza mara nyingi shinikizo hutoka kwa wamiliki wa majengo.

Mkandarasi mmoja, aliyeomba jina lake lisitajwe, anasema mmiliki anaweza kuagiza wazi sehemu ya chini ifunguliwe kwa biashara huku ujenzi ukiendelea juu.

“Kisheria mkandarasi anatakiwa kukabidhi jengo baada ya kukamilika na kukaguliwa, lakini kivitendo hali huwa tofauti. Mradi ni wa mwenye jengo,” anasema.

Anasema kutokana na hali hiyo, baadhi ya majengo huondoa mabango ya ujenzi ili yaonekane kana kwamba kazi imekamilika, wakati ujenzi unaendelea kwenye ghorofa za juu.

“Ukweli ni kwamba kuna wakati kazi inaendelea huku jengo tayari linatumika. Hili ni kosa, lakini mfumo unatufanya tufumbie macho,” anasema.

Kwa nyakati tofauti, Mwananchi imeitafuta Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) kwa simu na barua pepe Januari 15, 2026 kujua nafasi yao kwa kinachoendelea Kariakoo bila mafanikio lakini, Oktoba 31, 2024, alipoulizwa kuhusu ubomoaji na ujenzi wa majengo Kariakoo, Msajili wa CRB, Rhoben Nkori, alisema ukaguzi unaendelea kufanyika ili kuhakikisha makandarasi wanaohusika kwenye miradi ya ujenzi wana sifa stahiki na wanazingatia matakwa ya sheria.

Moja ya jengo linaloendelea kufanyiwa ukarabati Kariakoo.

Alisema CRB imejielekeza katika kusajili makandarasi bora, kuwajengea uwezo na kusimamia utekelezaji wa miradi ili ihakikishe majengo yanajengwa kwa viwango vinavyotakiwa.

“Lengo letu ni kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ubora na usalama, na makandarasi wanakuwepo kwenye miradi kwa muda wote wa ujenzi,” alisema Nkori.

Kwa upande wa Osha, Mwananchi iliwasilisha maswali yake kwa njia ya barua pepe Januari 15, 2025 na walijibu kuwa wameyapokea.

“Asante kwa kuwasiliana nasi, ujumbe tumepokea.” Hata hivyo, hadi tunaandaa habari hii hawakuwa wamejibu.