Polisi Yamkaribisha Kamishna Mkama kwa Ushindi

Bakari Mahundu
April 20, 2026
0 Comments

Kikosi cha Polisi Tanzania kimeibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Transit Camp ya Dar es Salaam katika mchezo wa Ligi ya Championship uliochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Shule ya Filbert Bayi mkoani Pwani.

Mabao ya Polisi Tanzania yalifungwa na mshambuliaji Tariq Seif pamoja na Denis Cuthbert, huku mchezo ukiwa na ushindani mkubwa kwa dakika zote 90.

Akizungumzia ushindi huo, Afisa Habari na Mawasiliano wa kikosi hicho, Inspekta Frank Lukwaro, amesema ushindi huo ni ukaribisho mzuri kwa Kamishna wa Polisi Jamii, CP Alex Mkama, ambaye ameteuliwa hivi karibuni kuongoza Kamisheni ya Polisi Jamii inayosimamia pia michezo.

“Ushindi huu ulikuwa muhimu kwetu ili kusogea hadi nafasi ya nne, lakini pia tangu Kamishna Mkama aanze kuongoza Kamisheni yetu huu ndio mchezo wa kwanza, hivyo ni zawadi kwake. Hii inaonesha kuwa mambo yataendelea kuwa mazuri hadi mwisho wa ligi,” amesema Inspekta Lukwaro.

Kwa ushindi huo, Polisi Tanzania imefikisha alama 45 na kujikita katika nafasi ya nne huku ikiwa imesalia michezo minane kabla ya ligi hiyo kumalizika.