. ******
Jumuiya ya Wanahabari wa Mitandao ya Kijamii (JUMIKITA) imetoa wito kwa vyombo vyote vya habari nchini kusitisha mara moja kumpa ushirikiano Madam Rita kufuatia kile kilichoelezwa kuwa ni kitendo kisicho na heshima wala uungwana dhidi ya chombo kimoja cha habari cha mtandaoni.
Kupitia taarifa aliyoutoa kwa niaba ya jumuiya hiyo, Mwenyekiti wake, Shaaban Matwebe, alisema JUMIKITA imesikitishwa na kulaani vikali tukio hilo, akisisitiza kuwa limekiuka misingi ya maadili ya taaluma ya habari.
Alibainisha kuwa kitendo hicho kinaashiria dharau, ukosefu wa adabu, pamoja na kutothamini mchango wa vyombo vya habari na wanahabari kwa jamii.
Matwebe aliongeza kuwa taaluma ya habari ni muhimili muhimu katika jamii, hivyo inapaswa kulindwa, kuheshimiwa na kuenziwa na wadau wote bila kujali nafasi au hadhi zao.
Kutokana na hali hiyo, JUMIKITA imeweka bayana kuwa ushirikiano na Madam Rita utasitishwa hadi pale atakapojitokeza hadharani kuomba radhi kwa umma pamoja na chombo cha habari kilichoathirika.