Dar es Salaam. Katika kipindi ambacho taasisi nyingi za kifedha zinakabiliwa na msukumo wa kuongeza faida, Benki ya NCBA Tanzania imeendelea kujitofautisha kwa kuonesha uthabiti wa kiutendaji na mwelekeo wa ukuaji wenye nidhamu.
Kwa mujibu wa taarifa za kifedha, jumla ya mali za benki hiyo ziliongezeka kwa asilimia 17.8, kutoka Sh512.8 bilioni mwaka 2024 hadi kufikia Sh604.0 bilioni mwaka 2025. Ukuaji huo unaashiria kuimarika kwa imani ya wateja pamoja na kupanuka kwa shughuli za benki katika sekta mbalimbali za uchumi.
Katika upande wa faida, NCBA Tanzania ilirekodi Sh16.1 bilioni, ikiwa ni ongezeko dogo la asilimia 0.6 kutoka Sh16 bilioni mwaka uliotangulia.
Ingawa ongezeko hilo linaonekana kuwa la wastani, linaakisi uimara wa benki katika mazingira yenye changamoto za kiuchumi, ikiwamo mabadiliko ya gharama za uendeshaji na ushindani mkali wa soko.
Mapato ya benki yalibaki imara yakifikia Sh50.5 bilioni 50.5, huku mapato yatokanayo na riba yakichangia Sh38.5 bilioni 38.5. Hii inaonesha msingi thabiti wa biashara unaotegemea zaidi huduma za mikopo na uwekezaji.
Mbali na takwimu za kifedha, mchango wa NCBA Tanzania katika uchumi halisi unaonekana kupitia huduma zake za kifedha zinazolenga sekta muhimu. Kupitia huduma za ufadhili wa mali (asset finance), benki imeendelea kusaidia sekta za biashara, usafirishaji na uzalishaji, ambazo ni mhimili wa ukuaji wa uchumi wa Tanzania.
Aidha, huduma za benki kwa kampuni (corporate banking) zimeendelea kuimarisha uhusiano na wateja wakubwa, huku uwekezaji katika huduma za kidijitali ukirahisisha upatikanaji wa huduma kwa wateja wengi zaidi.
Kwa kuwa sehemu ya mtandao mpana wa kikanda wa NCBA Group PLC, benki hiyo kwa mujibu wa matokeo ya kundi, jumla ya mali zake katika Afrika Mashariki zilifikia takribani Sh13.2 trilioni, huku faida kabla ya kodi ikiwa Sh515 bilioni na faida baada ya kodi Sh433 bilioni 433 kwa mwaka 2025.
Masoko ya kikanda, ikiwamo Tanzania, Uganda na Rwanda, yalichangia takribani Sh66.6 bilioni katika faida kabla ya kodi ya kundi, sawa na asilimia 13 ya mapato yote. Hii inaonesha kuongezeka kwa umuhimu wa masoko haya katika mkakati wa ukuaji wa NCBA Group.
Akizungumzia matokeo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa NCBA Group PLC, John Gachora, amesema: “Matokeo yetu yanaonesha nguvu ya mkakati wa ukuaji endelevu na uwekezaji katika biashara zetu kuu pamoja na kuimarisha uwepo wetu kikanda.”
Mkurugenzi Mtendaji wa NCBA Bank Tanzania, Alex Mziray, amesema: “Matokeo ya mwaka 2025 yanaonesha benki inayokua kwa nidhamu huku ikiendelea kuwahudumia wateja na kuwekeza katika maeneo ya kimkakati.”
Ameongeza kuwa sehemu ya kundi inaiwezesha benki hiyo kupata nguvu ya mtandao mpana, huku ikiendelea kutoa suluhisho linalolenga mahitaji ya soko la ndani.
Aidha zaidi ya mafanikio ya kifedha, benki hiyo inaendelea kuongozwa na falsafa ya Ubuntu, dhana inayosisitiza mshikamano na ustawi wa pamoja kwa lengo la kukuza uchumi jumuishi na kusaidia biashara ndogo na za kati.
