Kiungo amtibua Pedro, aitisha kikao cha ghafla

YANGA ilikuwa uwanjani jana usiku ikicheza mchezo wake wa kwanza kwenye Kombe la Muungano, lakini ile adhabu ya kufungiwa kwa kiungo wa timu hiyo, Mudathir Yahaya imemtibua kocha wa kikosi hicho, Pedro Goncalves, kisha akaitisha kikao.

Alianza kipa wa timu hiyo, Djigui Diarra kupewa adhabu ya kufungiwa mechi tatu na faini ya Sh4 milioni kutokana na makosa mawili tofauti ya utovu wa nidhamu aliyofanya katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mtibwa Sugar uliochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri Dodoma.

Kwa mujibu wa adhabu zilizotolewa na Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi zilizotangazwa Ijumaa, Machi 27, 2026, Diarra alitozwa faini ya Sh2 milioni na kifungo cha mechi tatu kwa kosa la kumshambulia refa wa mchezo huo, Gilbert Mrina wa Kilimanjaro. Pia akatozwa faini ya Sh2 milioni kwa kosa la kuonyesha ishara ya matusi mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo.

Baada ya hapo, baadhi ya mashabiki wa Yanga wakachukua jukumu la kuilipa faini hiyo kwa kuanzisha kampeni ya kumchangia.

Aprili 20, 2026 zikiwa zimepita takribani siku 24 tangu Diarra akumbane na adhabu hiyo, imetokea tena kwa Mudathir Yahya ambaye naye atazikosa mechi tatu kwa makosa ya kinidhamu, huku akitozwa faini ya Sh1 milioni ambayo pia mashabiki wa Yanga wameamua tena kuchukua jukumu la kulipa fedha hiyo.

Hali hiyo imetafsiriwa ni kama mashabiki hao wanafurahia wachezaji kufanya makosa ya kinidhamu ambayo mbali na faini wanazotozwa, pia wanatibua programu za benchi la ufundi kwa kukosekana kwao.

YANG 02

Iko hivi; Mudathir amefungiwa mechi tatu na Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB), kupitia kamati yake ya usimamizi ya ligi baada ya kubainika kumpiga kwa kiwiko mchezaji Pamba Jiji kwenye mchezo baina ya timu hizo lakini pia akipigwa faini ya Sh1 milioni.

YANG 04

Adhabu hiyo haitamzuia Mudathir kucheza mashindano ya Kombe la Muungano ambayo Yanga ilianza jana usiku, lakini atazikosa mechi za ligi kuanzia mchezo huo ujao wa Dabi ya Kariakoo ambapo Simba itakuwa mwenyeji wa Yanga, Mei 3, 2026.

Akizungumzia adhabu hiyo, Pedro amesema ameshtushwa na hilo akisema wala hakutarajia adhabu ya namna hiyo kwa kikosi chake kwasasa ambapo hata tukio husika hakuliona kwenye mechi hiyo mpaka alipokuja kuelezwa na wasaidizi wake.

Pedro amesema kukosekana kwa Mudathir kwenye mechi zao tatu zijazo ni pigo kubwa kwa kikosi hicho kutokana na ubora wake ambapo sasa anaanza kupiga hesabu mpya za nani ataziba pengo hilo.

“Nilishtuka sana niliposikia hiyo adhabu, kusema ukweli baada ya kufungiwa kwa Diara (Djigui) sikutegemea kama kutakuwa na kitu kama hicho, hata niliposikia hii ya Mudathir sikuliona hilo tukio mpaka wasaidizi wangu walipokuja kunikumbusha.

“Tuna timu nzuri na tuna viungo wazuri, tutaangalia ni nani anaweza kuja kuendelea pale ambapo tutamkosa Mudathir, tutatumia hizi mechi za Muungano kuweka mambo yetu sawa,” amesema Pedro.

Pedro amesema Mudathir alikuwa ameanza kutengeneza muunganiko mzuri ambapo amepanga kuwakumbusha wachezaji wake wote kuwa makini na matukio ya kinidhamu ambayo yanaipunguzia nguvu timu yao.

YANG 03

“Sitaki kuwalaumu sana wachezaji wangu kutokana na wakati mwingine kuna matukio wanasababishiwa lakini kitu muhimu hapa nataka kuzungumza nao kuwakumbusha wanaichezea timu kubwa ambayo wakati mwingine timu zingine zinakuja kwa akili ya kuwaharibia.

“Wanatakiwa kuwa makini, kucheza kwa kutambua kwamba kuna watu wanawatafutia makosa, adhabu kama hizi zinaleta presha kwa timu, nafahamu tuna wachezaji wazuri ambao wanaweza kuziba nafasi ya Mudathir lakini kuna raha kuwa na wachezaji wako wote,” amesema.

Kwa mujibu wa adhabu hiyo, mechi tatu ambazo Mudathir atazikosa ni dhidi ya Simba, KMC na Coastal Union ambazo zote za Ligi Kuu Bara.

YANG 01

Kitendo hicho kinachofanywa na mashabiki wa Yanga kuwachangia wachezaji wanapoadhibiwa kwa makosa ya utovu wa nidhamu, kimemuibua beki wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Amir Maftah akisema mashabiki kuwalipia wachezaji wanapoadhibiwa kwa utovu wa nidhamu, haoni kama kinaleta afya ya maendeleo na ustawi wa soka nchini.

Staa wa zamani huyo aliyeichezea Yanga 2007 na Simba 2010, amesema: “Kuzichangia klabu ama mchezaji anapokosea ni kuunga mkono na kuchochea matukio ya utovu wa nidhamu yazidi kuongezeka, nia ya vyombo vinavyosimamia nidhamu ni kuimarisha ustawi wa soka na siyo kumkomoa mtu.

“Nashauri kamati husika ziweke msisitizo wa mhusika wa adhabu anapaswa kuwajibika, ili kulinda sheria 17 za soka kama mashabiki wakikosea na wao pia watapaswa kuwajibika.”

Staa wa zamani wa Mecco ya Mbeya, Abeid Kasabalala ambaye kwa sasa ni katibu msaidizi wa Chama cha Wachezaji wa Mpira wa Miguu Tanzania (SPATA), amesema haungi mkono pindi adhabu za wachezaji zinapotolewa na mashabiki wanawalipia pesa, anaona kinaweza kikaendeleza utovu wa nidhamu.

“Hata sisi wakati tunacheza tulikuwa tunafanya makosa, kwani kuna wakati mwili unachemka ukajikuta umefanya maamuzi yasiyo sahihi, adhabu inapokuja inamkumbusha mchezaji anapokuwa katika harakati zake na mpira ajilinde na makosa ili soka liendelee kuwa salama,” amesema kiongozi huyo na kuongeza;

“Mashabiki wanapoyakingia mkono mambo hayo ni sawa na mtoto afanye kosa jirani akimuadhibu halafu atokee baba yake na kumkingia kifua kama hana makosa, huyo mtoto anaweza akawa anakosa nidhamu kila mara, hivyo nashauri elimu kwa wachezaji iendelee kutolewa mara kwa mara ya kuzijua kanuni zinazowahusu wakiwa mchezoni.”