Yanga yatangulia nusu fainali Muungano, ikiipiga Muembe Makumbi

YANGA imeanza vyema kampeni ya kutetea ubingwa wake wa Kombe la Muungano, ikiichapa Muembe Makumbi City kwa mabao 4-0.

Haikuwa mechi ngumu kwa mabingwa hao, ikitawala vizuri dakika zote 90, ikifunga mabao yake katika vipindi vyote viwili vya mchezo huo uliopigwa leo Aprili 21, 2026 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Mshambuliaji Prince Dube, ameendeleza moto wake wa kutikisa nyavu, akifunga bao la kwanza dakika ya 16, akitumia pasi safi ya kiungo Allan Okello.

MUU 01

Bao la pili kwa Yanga likapatikana dakika ya 34, baada ya beki wa Muembe Makumbi City, Suleiman Khamis, kujifunga wakati akipambana kuokoa mpira wa kichwa wa Shekhan Khamis.

Shekhan akaipa Yanga bao la tatu akipiga shuti Kkali la nje ya eneo la hatari akiunasa mpira uliotokana na krosi ya Shadrack Boka, uliotangulia kuguswa na beki wa Muembe Makumbi na kumkuta mfungaji, timu hizo zikienda mapumziko kwa bingwa mtetezi akitoka mbele kwa mabao 3-0.

MUU 02

Kipindi cha pili Dube tena akaipa bao la nne Yanga lakini likawa la pili kwake kwenye mchezo huo, akimalizia mpira uliotemwa na kipa Rashid Daimu wakati akiokoa shuti la mshambuliaji huyo.

Muembe Makumbi licha ya kujaribu kujenga mashambulizi lakini hayakuwa kitu kizito kwa ukuta wa Yanga.

Nafasi nzuri kwa Muembe Makumbi kwenye mchezo huo ilipatikana dakika ya 76, mshambuliaji Abdallah Pina akashindwa kumalizia krosi ya Mustapha Muhsin.

MUU 03

Ushindi huo wa Yanga unaipeleka hatua ya nusu fainali ya kwanza itakayopigwa Aprili 25, mwaka huu ikimsubiri mshindi wa mchezo wa robo fainali ya pili kesho kati ya Azam FC dhidi ya KVZ.