Dar es Salaam. Licha ya wanawake kuchangia karibu asilimia 40 ya nguvu kazi ya kilimo duniani na kuwa na mchango mkubwa nchini Tanzania, bado wanakabiliwa na changamoto za kimfumo, zikiwemo umiliki wa ardhi, mitaji, teknolojia, soko, upatikanaji mdogo wa huduma za kifedha, huduma za ugani na ushiriki katika uamuzi.
Hali hiyo imetajwa kupunguza uzalishaji, kushusha kipato cha kaya na kuathiri usalama wa chakula pamoja na lishe bora.
Kutokana na hali hiyo, Tanzania imeweka bayana umuhimu wa kushughulikia kwa haraka vikwazo hivyo vya muda mrefu vinavyowakabili wanawake katika sekta ya kilimo.
Tanzania imebainisha kwamba ukosefu wa fursa sawa katika umiliki wa ardhi, upatikanaji wa mitaji na teknolojia unaendelea kudhoofisha uzalishaji na kuongeza tatizo la uhaba wa chakula katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini.
Kauli hiyo imetolewa leo, Aprili 21, 2026 wakati wa mkutano wa ngazi ya juu uliowakutanisha maofisa wa serikali, wadau wa maendeleo na wawakilishi kutoka nchi mbalimbali za kanda hiyo, ukiwa na lengo la kuharakisha utekelezaji wa sera za kilimo zinazozingatia usawa wa kijinsia.
Akizungumza katika uzinduzi wa kikanda wa Mwongozo wa Hiari wa Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wa Wanawake na Wasichana (VG-GEWGE) ulioandaliwa na Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Peter Msoffe, amesema kuwawezesha wanawake si suala la haki tu, bali pia ni kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi na mageuzi ya mifumo ya chakula.
Mwakilishi wa Shirika la FAO nchini Tanzania, Tipo Nyabenyi akizunguma leo kwenye uzinduzi wa kikanda wa Mwongozo wa Hiari wa Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji wa Wanawake na Wasichana (VG-GEWGE) jijini Dar
Amesema wanawake wakipewa fursa sawa ya kumiliki rasilimali za uzalishaji na kushiriki katika uamuzi, mavuno yanaweza kuongezeka kwa asilimia 20 hadi 30, hali itakayoboresha maisha na kupunguza njaa.
Aidha, licha ya uzalishaji kuwa wa kutosha, kaya nyingi bado zinategemea lishe duni inayotegemea zaidi nafaka.
“Lishe zisizo na mchanganyiko wa kutosha wa matunda, mboga mboga na vyakula vya protini hushindwa kukidhi mahitaji ya virutubisho muhimu hasa kwa watoto,” amefafanua.
Akisisitiza dhamira ya Serikali, Msoffe ametaja mifumo muhimu ya sera, ikiwemo Sera ya Taifa ya Jinsia na Maendeleo ya Wanawake ya mwaka 2023, Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050 na Sera ya Kilimo ya mwaka 2013, pamoja na ahadi za kimataifa kama Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) na Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika.
Hata hivyo, pamoja na kuwepo kwa sera hizo, bado kuna pengo katika utekelezaji kutokana na ukosefu wa rasilimali, mifumo dhaifu ya utekelezaji na mila na desturi zinazokwamisha usawa wa kijinsia.
Naibu Katibu huyo ametoa wito kwa nchi wanachama kujumuisha mwongozo wa VG-GEWGE katika mikakati ya kitaifa, kuimarisha mifumo ya takwimu na kuwekeza katika kujenga uwezo.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) nchini Tanzania, Tipo Nyabenyi, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano katika kujenga mifumo jumuishi ya chakula.
Amesema ingawa wanawake wengi barani Afrika wanajihusisha na mifumo ya uzalishaji chakula, bado wanakabiliwa na ukosefu wa usawa unaodhoofisha uwezo wao.
“Changamoto hizi haziwaathiri wanawake pekee, bali pia zinakwamisha maendeleo ya jumla ya usalama wa chakula na uchumi,” amesema.
Mwongozo wa VG-GEWGE ni hatua muhimu inayotoa suluhisho la vitendo katika kushughulikia changamoto za kimfumo, kupanua upatikanaji wa rasilimali na kuimarisha uongozi wa wanawake.
Kwa upande wake, Mratibu wa Taifa wa Masuala ya Jinsia na Wanawake, Shirika la FAO, Jane Msagati, amesema wanatamani kuona maelekezo ya mwongozo ulioanzishwa na Kamisheni ya Usalama wa Chakula Duniani yanatumiwa nchini Tanzania ili kumwezesha mtoto wa kike na kuboresha usawa wa kijinsia.
Amesema mwongozo huo umesimama katika masuala ya lishe, uongozi na jamii, pamoja na kuhusika kwa wanaume katika kushirikisha wanawake kupata usawa katika umiliki wa rasilimali na kufanya uamuzi.
Ameongeza kuwa usalama na mgawanyo wa chakula ndani ya nyumba na jamii unaleta matokeo chanya.
Amesema mwongozo huo, bila kusahau, unasimamia matokeo chanya ya lishe, ambapo lishe haipaswi kuleta matokeo hasi, ikiwemo masuala ya utapiamlo.
