Video ya CCTV Ikimuonesha Bodaboda Aliyeiba Mtoto Mwanza, Apatikana Akiwa Hai

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limefanikiwa kumpata mtoto wa kike mwenye umri wa miaka mitatu na miezi kumi aliyeripotiwa kuibwa Aprili 18, 2026 katika eneo la Kona ya Bwiru, Wilaya ya Ilemela.

Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi, mtoto huyo aliibwa majira ya saa 5:00 asubuhi akiwa na mama yake, Neema Julius Sesela (19), mkazi wa Nyampala “B”, Kata ya Nyamanoro, Wilaya ya Ilemela. Inadaiwa mtu asiyejulikana alimchukua mtoto huyo na kuondoka naye kwa kutumia pikipiki yenye namba zisizofahamika.

Baada ya mama wa mtoto kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi Kirumba, uchunguzi ulianza mara moja. Polisi walipata picha za CCTV kutoka kwa mkazi mmoja wa eneo hilo zikimuonesha mwanaume akiondoka na mtoto huyo kwa pikipiki, ingawa namba za usajili hazikuonekana vizuri.

Msako wa Polisi kwa kushirikiana na wananchi uliendelea hadi Aprili 20, 2026 majira ya saa 3:30 usiku, ambapo taarifa zilipatikana kuhusu mtoto wa kike aliyetelekezwa katika makaburi ya Nyasaka, Wilaya ya Ilemela. Mtoto huyo aliokotwa na wasamaria wema na kupelekwa kwa mwenyekiti wa mtaa wa Nyamuge, Kata ya Nyasaka.

Polisi walifika eneo hilo na kumkuta mtoto akiwa na michubuko usoni kabla ya kumpeleka Hospitali ya Rufaa ya Sekou-Toure kwa uchunguzi zaidi. Wazazi wake, Neema Julius Sesela na Mwankunja Edward (30), fundi seremala na mkazi wa Nyampala “B”, wamemtambua mtoto huyo kuwa ni wao.

Wakati huo huo, Polisi Mkoa wa Mwanza wanaendelea kumtafuta mtoto mwingine mwenye umri wa miezi 10 aliyeibwa Aprili 19, 2026 katika mtaa wa Bukala, Kata ya Ibisabageni, Wilaya ya Sengerema.

Mama wa mtoto huyo, Levina Daud Leonard (32), mkulima na mkazi wa Bukala, aligundua mtoto wake ameibwa akiwa nyumbani kwake na kutoa taarifa Polisi. Hadi sasa mtoto huyo hajapatikana na juhudi za kumtafuta pamoja na kumsaka mtuhumiwa zinaendelea.

Katika tukio jingine, watu wawili wamezama baada ya mtumbwi waliokuwa wakitumia kugongwa na meli katika Ziwa Victoria, eneo la Mihama, Wilaya ya Ilemela.

Tukio hilo lilitokea Aprili 17, 2026 majira ya saa 2:00 usiku wakati meli ya MV Uhuru, mali ya Kenya Railways Corporation, ikitokea Bandari ya Mwanza Kusini kuelekea Kisumu nchini Kenya, ilipougonga mtumbwi uliokuwa umebeba wavuvi wanne.

Baada ya mtumbwi huo kupinduka, wavuvi wawili waliokolewa huku Noel Julias na Peter Masanja wakizama majini. Aprili 20, 2026 mwili wa Peter Masanja ulipatikana, huku juhudi za kumtafuta Noel Julias zikiendelea.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limetoa wito kwa wazazi kuendelea kuwa na usimamizi wa karibu kwa watoto wao na pia kuwataka wananchi kutoa taarifa zitakazosaidia kupatikana kwa mtoto wa Sengerema pamoja na mtu anayesakwa katika tukio hilo.